Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa
Juma Khamis ambaye alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Mkoa
wa Dodoma kwa makosa mawili yanayohusu rushwa, amekosa dhamana mpaka
Jumanne ijayo kwa hofu ya kuingilia mchakato wa uchaguzi mkuu wa umoja
huo .
Sadifa
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Zanzibar alifikishwa mahakamani
hapo majira ya 4:55 asubuhi na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akisoma
kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Joseph Fovo,
mwendesha mashtaka wa Takukuru, Biswaro Biswaro alisema mshtakiwa huyo
alitenda makosa hayo Desemba 9, mwaka huu akiwa nyumbani kwake maeneo ya
kata ya Mnadani, Manispaa ya Dodoma.
Alisema
katika kosa la kwanza, Sadifa akiwa nyumbani kwake alitoa rushwa ya
vinywaji kwa wajumbe ili wamchague mgombea wa nafasi ya Makamu
mwenyekiti wa UVCCM, Rashid Mohamed Rashid.
Biswaro
alisema kosa la pili analokabiliwa nalo Sadifa ni kutoa ahadi ya
kuwalipia gharama za usafiri wajumbe hao kutoka Dodoma–Kagera kama
zawadi kwao baada ya kumpigia kura mgombea huyo.
Wakili
huyo aliwataja wajumbe hao kuwa ni Kadogo Shabani, Abdallah Hamimu,
Octavian Andrea, Didas Zimbihile, Tasinta Nyamwiza, John Lufunga,
Mtwawafu Kantangayo, Haleluya Ivody, Deocres Kagunila, Emmanuel
Shitobelo, Happiness Rynyogote, Adolf Andrew, Adinani Musheruzi, Editha
Domisian na Hashim Abdallah.
Biswaro
alisema mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kinyume na Sheria ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15(1)(b) na
(2).
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Fovo alimhoji mshtakiwa huyo ambaye alikana kutenda makosa yote mawili.
Biswaro alisema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na upande wa Jamhuri unaweka pingamizi la dhamana kwa mshtakiwa.
Mwendesha
mashtaka Biswaro alisema sababu za kuzuia dhamana ya mshtakiwa huyo ni
kutokana na mkutano mkuu wa uchaguzi UVCCM kuwa wa siku mbili mfululizo,
juzi na jana na pia matokeo yakiwa bado hayajatangazwa.
Alisema endapo Sadifa atakuwa nje kuna uwezekano wa kuingilia uchaguzi huo.
“Naomba
Mahakama itambue uchaguzi bado unaendelea na mshtakiwa hadi sasa
hajakabidhi uongozi... bado ni mwenyekiti,” alisema Biswaro.
Aidha,
Biswaro alisema sababu nyingine ni kuwa mashahidi wengi ni viongozi
ambao ni wenyeviti na makatibu na endapo akiachiwa kwa dhamana ana kila
aina ya ushawishi unaoweza kuvuruga upelelezi.
Kufuatia
maelezo hayo, wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga alipinga kuzuiwa kwa
dhamana na kudai kuwa ni haki ya mtu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Alibainisha
kiapo cha kuzuia dhamana hicho kilichowasilishwa mahakamani ambacho
kimetolewa na Kamanda wa Takukuru mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga, hakina
mashiko.
“Uchaguzi
wa UVCCM umeshaisha na mshindi tayari ameshapatikana na hakuna uchaguzi
mwingine wa kuingilia au kama kuna uchaguzi utafanyika, kiapo
kingesema,” alisema Wasonga.
Alihoji sababu za kupelekwa mahakamani kwa kesi ambayo upelelezi wake haujakamilika na kuzuia dhamana kwa mshtakiwa.
Alisema
mshtakiwa huyo hataweza kuingilia uchunguzi kwa sababu
walizozitoa.“Hawa mashahidi atawezaje kuwashawishi wakati mtu ameshatoka
madarakani?" Alihoji wakili Wasonga."Mteja wangu ni Mbunge, ni mtu
makini na anaaminiwa. Asihukumiwe kwa kuwekwa ndani kwasababu zisizo na
mashiko.”
Aliomba
mahakama itupilie mbali pingamizi hilo na mshtakiwa apewe dhamana kwa
kuwa hataweza kuingilia uchaguzi kwa kuwa uchaguzi mwingine wa UVCCM
utafanyika mwaka 2022.
Kutokana
na mvutano huo wa kisheria, Hakimu Fovo aliahirisha kesi hiyo hadi
Jumanne ijayo ndipo mahakama itatoa maamuzi kuhusu suala hilo. Alisema
mshtakiwa ataendelea kuwa rumande.
0 comments:
Post a Comment