Mchekeshaji maarufu Bongo, Amri Athumani alimaarufu kama 'Mzee Majuto'
amefunguka na kuweka wazi ugonjwa ambao unamsumbua kwa sasa kuwa ni tezi
dume na kudai kuwa atafurahi sana endapo atafanyiwa upasuaji na
kuondolewa maradhi hayo.
Mzee Majuto ambaye kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam na tayari ameanza
hatua za awali kuhakikisha kuwa anafanyiwa upasuaji kuondolewa tezi dume
amesema kuwa kutokana na umri wake hashangazwi yeye kupata ugonjwa huo
na kudai ni ugonjwa tu kama yalivyo magonjwa mengine.
"Tayari nimeshafanyiwa vipimo kadhaa toka nilipofikishwa Muhimbili hapa
saizi nasubiri siku ya Jumanne niende kuonana na daktari ambaye
anashughulika zaidi na tezi dume ili aweze kusoma vipimo hivyo vizuri na
kuona jinsi gani naweza kufanyiwa upasuaji. Huu ni ugonjwa wa kawaida
na wapo watu wengi wameshaupata hata wengine nyinyi mnawajua sema mimi
sitaki kuwataja tu hapa" alisema Mzee Majuto
Aidha Mzee Majuto ameshauri watu wengine ambao wana ugonjwa huo wa tezi
dume kuhakikisha wanafanyiwa upasuaji mapema kabla ya njia za mkojo
kuziba kwani ikifika hatua hiyo watapata shida sana.
Mwaka jana Mzee Majuto alifanyiwa upasuaji akiwa mjini Tanga alipokuwa
akisumbuliwa na ugonjwa wa 'Hernia' lakini mwaka huu ameamua kuja
Muhimbili jijini Dar es Salaam kufanyiwa upasuaji wa Tezi dume kutokana
na ushauri wa madaktari baada ya kugundua kuwa ana tatizo la moyo.
0 comments:
Post a Comment