Wednesday 31 January 2018

ZIZZOU KATIKA IMANI YA NAHODHA EDWARD JOHN SMITH


Na Raphael Mwenda
                                   Mnamo mwaka 1909 kampuni ya RMS Titanic ilitengeneza meli ya kihistori iliyochukua miaka takribani minne kukamilisha matengenezo yake. Mnamo tarehe 10 mwezi wa nne mwaka 1914 TITANIC ilifanya safari yake ya kwanza kutoka pale Southampton England kuelekea New York  Marekani katika safari yake hiyo Titanic ilibeba jumla ya abiria 2000 huku ikiongozwa na nahodha Edward John Smith. Ikiwa katika mwendo mkali mnamo tarehe 15 mwezi wa nne mwaka 1912  siku tano katika safari na siku moja kabla ya kufika pale Pier 54 jijini New York Titanic ilipata ajali na kuzama maelfu ya watu walipoteza uhai inakadiliwa kuwa zaidi ya watu 1500 walipoteza maisha kati ya watu hao miongoni mwao alikuwamo Nahodha Edward John Smith ambae hakukubali kuicha meli ile.

                                   Mnamo juni mwaka 2001 Frolentino Perez alituma fax kwenda katika klabu ya Juventus pale Italy fax ile ilikua ikihitaji kujua thamani ya ununuzi wa Zinedine Zidane baada ya kupokea fax ile rais wa Juventus bwana Victorio Caissoti di Chiusano alitoa jibu rahisi tu "Zizzou hauzwi" lakini kwa kiburi na jeuri ya Frolentino Perez alirudisha jibu kwa kusema hakuna mchezaji asieuzwa ulimwenguni na kuweka ofa ya pauni milioni 46.2. Ndio ni binadamu gani angeikataa pauni milioni 46.2 kwa kipindi kile hata bwana Victorio alishindwa kukataa na hatimae Zinedine Zidane alikwenda kujiunga na Real Madrid Zinedine Zidane alikuwa mchezaji ghali duniani kwa wakati huo.


                                  Si Florentino Perez pekee bali ulimwengu mzima hakuna aliesahau 'volley' iliyowapa Real Madrid taji la tisa la ulaya kwa kuikandamiza Bayer Leverkusen katika dimba la Olimpic pale pale Ujerumani katika ardhi yao ndio Zinedine Zidane aliibuka shujaa kwa goli lake la dhahabu. Kuanzia pale na kuendelea Zizzou alikua kipenzi cha mashabiki na viongozi wa pale Santiago Bernabeu alijizolea umaarufu kila kona ya dunia. Katika kipindi chake chote cha soka Zizzou ameshinda mataji yote katika ngazi ya klabu na timu ya taifa pia. Ndio Kombe la dunia mwaka 1998 pale ufaransa katika ardhi yao ya nyumbani au mwaka 2000 pale Brussel akichukua kombe la mataifa ya ulaya.
                                  Kwa mafanikio na mchango wake katika kikosi cha Real Madrid mnamo mwaka 2006 Zizzou alistaafu soka na kujikita katika masomo ya ukocha lakini pia Real Madrid ikampa kazi ya kusaka vipaji katika kona tofauti za ulaya katika kazi hii mpya alifanikiwa kwa kiasi fulani kwani Raphael Varane ni tunda la juhudi zake katika kusaka vipaji. Baada ya kuhitimu mafunzo ya ukocha Zizzou alikabidhiwa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18 pale Madrid huku kocha mkuu wa timu ya wakubwa akiwa José Mourinho aliejiunga Madrid akitokea Inter Milan ya kule Italia. 

                                  Baada ya Jose Mourinho kufungashiwa virago pale Santiago Bernabeu kazi ya kuwa kocha mkuu alikabidhiwa Carlo Ancelotti akitokea kule Paris Saint German (PSG)ya ufaransa. Alipofika Madrid Ancelloti alimuhitaji Zizzou kuwa msaidizi wake katika benchi la ufundi la Madrid. Walifanya kazi kwa mafanikio katika misimu miwili wakiweza kupata taji la ligi ya mabingwa ulaya kwa kuwa chapa mahasimu wao wa Madrid Atletico de Madrid pale Lisbon ureno pia waliweza kuchukua Spanish copa del rey lakini katika msimu uliofuata Madrid alikua na msimu mbovu na mabosi wa Madrid wakiongozwa na Florentino Perez hawakufikiria mara mbili zaidi ya kumfuta kazi Ancelloti na mikoba yake kukabidhiwa Rafa Benitez huku Zizzou akipewa kazi ya kufundisha timu ya vijana Real Madrid Castilla.
                                      Muenendo mbovu wa timu na maelewano mabaya kati ya Benitez na wachezaji wa Real Madrid haikuchukua muda mrefu kwa Madrid kumfuta kazi Rafa na jibu lao la haraka ilikua ni Zinedine Zidane 'Zizzou' katika staili ya kipekee Zizzou aliiongoza Real Madrid katika safari ya kuchukua kombe la Ligi ya mabingwa ulaya pale Giuseppe Meaza kwa kuwafunga tena mahasimu wao Atletico de Madrid katika mikwaju ya penati baada ya kutoka sare ya goli moja moja.
                                      Kila kitu katika maisha ya soka Zizzou amekipata utukutu ule wa Sergio Ramos yeye amekwisha mfanyia Marco Materrazi pale Ujerumani katika mechi muhimu kabisa ya fainali ya kombe la dunia mwisho wa yote Zizzou akiwa mchezaji muhimu katika kikosi alilimwa kadi nyekundu na kutoka uwanjani timu ikiwa inamuhitaji kuliko kitu chochote kile zile pasi za Luka Modric yeye amekwisha wapigia sana akina Raul Gonzalez na akina Thienry Henry yale mashuti ya Tony Kroos yeye amekwisha yapiga sana katika ubora wake zile chenga za Christian Ronaldo yeye ameshawafanyia sana mabeki visiki akina Ricardo Canavaro katika ubora wao ile bei ya Gareth Bale yeye ndie alikua mchezaji wa kwanza kununuliwa kwa bei mbaya na Real Madrid zile ballon d'Or za Ronaldo yeye ameshazichukua kabla yake je ni mchezaji gani atakaeambiwa na Zizzou fanya hivi na vile na akakataa? Hapa bado sijamuona kwa maana yale wanayoyafanya yeye amekwisha yafanya kabla yao.
                                        Msimu wake mzima akiwa kocha mkuu pale Santiago Bernabeu Zizzou alishinda kila kitu La Ligi na akaenda kuweka rekodi ya kuchukua ligi ya mabingwa ulaya kwa mara ya pili mfululizo safari hii akiwaaibisha vibibi vizee wa Turin Juventus pale Cardiff Wales nyumbani kwa Gareth Bale.  Jose Mourinho na vijana wake kumi na moja uwanjani walipagawa kwa soka tamu na la kuvutia walilochezewa na vijana wa Zizzou kule Macedonia katika mchezo wa UEFA Super Cup  Real Marid waliondoka kifua mbele. Katika kombe la Spanish super cup Barcelona walichezewa soka la hali ya juu na vijana wa Zizzou na kila shabiki wa soka aliamini Madrid hii haitasimamishwa.
                                     Kosa la Titanic kuzama si Nahodha Edward John Smith bali ni mhandisi wa meli ile bwana Bruce ambae alihitaji meli ile kwenda kwa kasi zaidi ili iweke rekodi ya kuwahi kufika pale New York matokeo yake meli iligonga mwamba katika usiku ule na watu wengi kupoteza maisha japo muhandisi yule alipona lakini nahodha Edward John Smith alipoteza maisha ndicho kinachokuja kuikumba Real Madrid na nahodha akiwa Zinedine Zidane. Katika dirisha la usajili mwezi juni mwaka 2017 Zizzou alitamka wazi kutomuhitaji Gareth Bale na kumuhitaji Kylian Mbappe katika kikosi chake lakini mwisho wa yote Frolentino Perez aliwaleta Dani Ceballos kutoka Real Betis kuja kumsaidia Toni na Luca katika ya uwanja akimleta Theo Hernandez kuja kumsaidia Marcelo akamrudisha Borja Maryol kuja kumsaidia Benzema pale mbele katika ushambuliaji.

                                         Benzema kachoka Ronaldo umri umekwenda akili yake inataka lakini miguu imechoka Luka Modric yeye amechoka kabisa nahodha Sergio Ramos amechoka umri umekwenda na bado anamaamuzi ya kitoto yanayoighalimu timu Gareth Bale anashinda katika vitanda vya hosipitali kila kukicha Madrid ilihitaji wachezaji wa kiwango cha dunia kuja kuongeza nguvu katika kikosi chao si wachezaji wale wa kawaida waliokwenda kuwa sajili. Lakini mzigo huu wa lawama kamwe hawezi kubebeshwa Perez bali Zizzou anaefanya kazi ya kuwaongoza wachezaji hawa.
                                     Nauona msimu mwingine wa njaa kwa Real Madrid kwani mbio za ubingwa wa la liga zimekwisha kwa tofauti ya alama kati yao na Barcelona alama 19 si rahisi kwao kuzikuta tena alama hizi katika kombe la mfalme nako wameshatolewa na Depotivo Leganes  huku katika ligi ya mabingwa wakikabiliwa na mfupa mgumu wa kuumeza dhidi ya PSG. Kibarua cha Zizzou kipo matatani lakini anakwenda kuumia peke yake kwa kuficha makosa ya mtu mwingine. Najaribu kumfikiria nahodha Edward John Smith naamini alikua na uwezo mkubwa sana wa kuokoka katika janga lile lakini aliwaza je dunia itamuangaliaje kwa kupoteza uhai wa maelfu ya watu waliokuwamo ndani ya meli ile? Je watamsamehe? Ili kuepusha yote hayo alipiga moyo konde akakaza roho na akazama na meli kwani makosa alishayafanya kwa kukubali kuongeza mwendo wa meli ile. Zizzou amekubali kuzama na jahazi la Real Madrid kwakua alishakubali kufundisha wachezaji ambao hakuwahitaji mwanzo. katika filamu ya Titanic walimuonesha bwana Bruce akiiangalia meli ile kwa masikitiko huku ikizama lakini alishukuru kwa yeye kubaki hai na kupona katika janga lile. Katika sehemu ya watu maarufu pale Santiago Bernabeu namuona Frolentino Perez akiiangalia Real Madrid ikizama taratibu huku akijua wazi Zizzou amekwisha lakini yeye chanzo cha haya yote anafuraha na kujipanga kuingia katika kinyang'anyiro kingine cha uchaguzi wa urais pale Madrid.

0 comments:

Post a Comment