Monday 29 January 2018

NAOMBA KAHAWA NIENDELEE KUMSIKILIZA ANTONIO CONTE


Na: Raphael Mwenda.
                            MNAMO mwaka 1583 mfizikia kutoka nchini Ujerumani bwana Leonhard Rauwolf aligundua kahawa. Katika maneno yake Leonhard anasema kahawa humsaidia mwanadamu katika kutibu magonjwa kadha wa kadha kama vile tumbo lakini pia inaongeza nguvu na kubwa hasa inapoteza usingizi. Kutoka miaka hiyo mpaka leo 2018 kahawa bado ni kinywaji maarufu na pendwa sehemu mbalimbali za dunia.
                                                                         Leonhard Rauwolf
                           Sitamani kabisa kulala siutamani usingizi ndio kwanini nilale ikiwa kuna hadithi tamu zilizojaa maneno ya kusisimua kutoka kwa raia wa Italia aishie pale London. Kwanini nilale ikiwa mzee huyu machachari anakila sababu ya kunifanya niongeze kikombe cha kahawa kila baada ya lisaa. Ndio ananiumiza tumbo kila nisikiapo habari zake nakosa nguvu kila nionapo tetesi zake usingizi unanikaba kabisa pale ninapoona na kusikia akikimbia kivuli chake.

                           Mnamo mwaka 2016 klabu ya Chelsea ilimtambulisha kocha Antonio Conte kuwa kocha mkuu pale Stanford bridge akichukua nafasi ya Jose Mourinho alietimuliwa miezi sita kabla. Ndio Conte alikuja uingereza akiwa ametoka katika timu ya taifa ya Italia lakini kabla ya hapo alikua kocha mkuu pale Juventus. Mafanikio yake kila mpenzi na shabiki wa soka ulimwenguni ama hakika anayafahamu vyema. Antonio Conte si kocha wa kubeza.
                            Baada ya kukabidhiwa timu Conte alihitaji kutumia mfumo wa 4-2-4 hivyo alihitaji kusajili mshambuliaji mwingine ambae angekuja kuwaongezea nguvu Hazard,Diego Costa pamoja na Pedro kwa kusikia kilio chake bodi ya Chelsea ilimsajili Michy Batshuayi kutoka Olympic de Marseille kwa ada ya paun 33.2. Batshuayi ametoka Marseille akiwa na magoli 26 katika mechi 62 si rekodi mbaya sana hasa ukizingatia umri wake wa miaka 22 kwa wakati huo. Conte alihitaji kiungo wa kuja kusaidiana na Nemanja Matic na pia beki wa kati pamoja na pembeni wote hawa alipewa akiletewa Ngolo kante kutoka Leicester city kuwa kiungo wake David Luiz akarudishwa kucheza na Gary Cahill pale katikati Marcos Alonso pia akaja kuongeza nguvu upande wa kushoto.
                           Bahati nzuri kwa Conte Chelsea haikua katika ligi ya mabingwa msimu ule wa 2016/2017 hivyo mlolongo wa mechi zake ulikua ni wiki baada ya wiki ilikua ratiba nzuri sana na yenye kila aina ya mapumziko kwaajili ya kujiandaa na mechi ijayo. Conte hakuwahi kulalamika kuhusu upangaji wa ratiba za ligi kuu uingereza wala hakuwahi kufikiria mwezi February atafanyaje kutokana na uchovu wa wachezaji katika ligi kuu ambao atalazimika kuwatumia katika michezo ya ligi ya mabingwa ndio kwanini awaze ikiwa alikua hana michuano mingi. Hatimae ligi ikaisha Chelsea akiwa bingwa Conte akiondoka kifua mbele mbele ya makocha wenzie ambao nao pia walipata vibarua msimu huo.
                            June ya mwaka 2017 wachezaji wengi wakiwa na timu zao za taifa mara Diego Costa wa Hispania aliibuka na kusema Antonio Conte anadharau kwani alimtumia ujumbe mfupi na kumwambia alikua haitajiki tena pale Stanford bridge. Diego Costa aliekua mfungaji bora wa Chelsea katika msimu uliopita haitajiki tena kwanini? Antonio alijitetea kwa kusema Diego hakua mwenye nidhamu ndio sote tunakubali Costa ni mtukutu haswaa lakini utukutu huu ndio silaha yake kubwa mbele ya mabeki wenye roho mbaya pale uingereza utukutu wake ulikua ukikupa uhakika wa magoli zaidi ya 15 kila msimu lakini Antonio hakuliona hilo yeye hakumuhitaji tena Diego Costa. Akili na macho ya Conte vilimuona Romelu Lukaku kama mbadala halisi wa Costa lakini kwa bahati mbaya Lukaku alikwenda Manchester United na Antonio aliamua kumchukua Alvaro Morata kutoka Real Madrid mchezaji aliewahi kufanya nae kazi kule Juventus. Baada ya kumuacha Costa hatimae Antonio alimuachia tena Nemanja Magic kwenda manchester united na nafasi yake ikazibwa na Tiemoue Bakayoko kutoka Monaco pamoja na nyongeza ya Danny Drinkwater kutoka Leicester city haikua mwisho bali mwanzo tu kwani Chelsea ilimsajili beki Antonio Rudiger kutoka Roma kuja kuongeza nguvu katika safu yao ya ulinzi pamoja na Zappacosta kutoka Torino ya Italia.
                           Ligi ilianza kwa mshangao mkuu kutoka kwa vijana wa Sean Dyche ndio waliwashangaza Chelsea pale pale darajani kwa kuchapwa goli tatu kwa mbili huku muamuzi akitoa kadi mbili nyekundu kwa Chelsea. Kilikua kipogo cha kusahau kwani timu ilicheza vizuri mechi zinazofuata na hatimae ligi ya mabingwa ulaya ikaanza mashabiki wa Chelsea wakifurahia ushindi dhidi ya vibonde wa kundi C Qarabag FK vijana wa Conte waliongoza kundi baada ya Roma kutoka sare na Atletico de Madrid. Raha ilinoga pale Chelsea alipotakiwa kucheza jumatano na Atletico de Madrid alafu jumapili acheze pia na Manchester city katika ubora wao, mechi dhidi ya Atletico walishinda lakini walipokuja kufungwa na man city pale Stanford bridge hatimae Antonio alinyanyua kinywa chake na kudai ana kikosi kidogo hivyo wachezaji wake walitumia nguvu nyingi kushinda dhidi ya Atletico na kuelekea mchezo ule walikua wamechoka.
                 Maswali yanakua mengi kuliko majibu inakuaje kikosi hakitoshi ikiwa waliuzwa wachezaji wenye ubora na akaleta wake alioamini ni sahihi kwa mfumo wake katika timu. Siku zimekwenda huku Antonio akiendelea na lawama zake na hatimae dirisha la usajili limefunguliwa na li karibuni kufungwa. Hapa sasa utafurahi tumbo litakuuma na nguvu pia zitakuishia Chelsea ilimsajili Ross Barkley kutoka Everton ili kuongeza nguvu katika eneo la kiungo mchezaji huyu anasajiliwa Chelsea akiwa hajacheza mchezo wowote kwa muda wa miezi tisa anakwenda kusaidiana na Bakayoko ambae Conte anamuona hayupo katika ubora pia Conte huyu huyu aliemuona Diego Costa hafai akamleta Alvaro Morata na Michy Batshuayi anaona bado hawatoshi na kutaka kuongeza mshambuliaji mwingine hapa sasa tumbo ndipo linavurugika kabisa unaposikia jina la Andy Carroll Peter Crouch pamoja na Eden Dzeko nachelea kuuliza kwanini Diego aliachiwa aondoke Chelsea kwanini Magic alipewa ruhusa ya kwenda Manchester? Kuna wachezaji wenye hadhi ya kuwa mahala fulani binafsi sioni Andy Carroll akiwa na thamani ya kuichezea Chelsea simtazami Peter crouch katika jicho la kuisaidia Chelsea.
                  Bado siku mbili dirisha la usajili January 2018 kufungwa na Antonio aliekua akilalama kuhusu ugumu wa ratiba na ufinyu wa kikosi amesajili mchezaji mmoja tu mwezi February kuelekea March Chelsea itakua na michezo iliyofungamana akianza na Manchester city pale Etihad kisha atasafiri kwenda Camp Nou kukipika na Barcelona katika usiku wa mabingwa akirudi atahitajika kwenda Turf Mor kumenyana na Burnley kisha atarudi Stanford bridge kuwa subiri Barcelona tena kabla ya kwenda Old trafford kuonana na vijana wa Jose Mourinho. Sitamani kulala asante  Leonhard Rauwolf kwa ugunduzi wako wa kahawa maana matatizo ya tumbo uchovu na usingizi vinaniandama ikiwa sitaki kuukosa uhondo huu wa filamu ya Antonio Conte pale Stanford bridge. Muhudumu naomba kikombe kingine cha kahawa.

0 comments:

Post a Comment