SOURCE MWANANCHI
Ungetegemea kuona watu wanaokwenda Nairobi
kumjulia hali mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu wakirudi na amani
kwamba wamekuta anaendelea vizuri, lakini ni tofauti; wanaonekana
jasiri zaidi na tayari kwa mapambano.
Ndivyo ilivyokuwa
kwa Mchungaji Peter Msigwa, Zitto Kabwe, Lazaro Nyalandu, Julius
Mtatiro na Sheikh Ponda Issa Ponda waliporejea kutoka jijini humo
kumjulia hali mwanasheria huyo mkuu wa Chadema.
Lissu,
ambaye amelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, alishambuliwa kwa
risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari lake
nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma.
Alihamishiwa
Nairobi usiku wa siku ya shambulio hilo linaloonekana lililenga kuchukua
maisha yake, na kwa mujibu wa wanaokwenda kumjulia hali, afya yake
inazidi kuimarika.
Lakini, jambo moja ambalo
limeonekana kwa wengi waliomjulia hali ni kauli zao baada ya kurejea;
wanaonekana sasa hawaogopi kifo, wako tayari kupambana na yeyote
wanayedhani ni adui, wameongezeka ujasiri na si waoga katika kuzungumza.
Wengi wao waliporudi walizungumza kwa ujasiri zaidi na hata walipozungumza na Mwananchi walionekana kusimamia kauli zao.
“Ukizungumza
na Lissu, usipopata ujasiri basi unapaswa ujiulize mara mbili juu ya
uwepo wako katika siasa,” anasema Mchungaji Msigwa, ambaye ni mbunge wa
Iringa Mjini kwa tiketi ya Chadema.
Msigwa anasema
alivyokutana na hali ya Lissu na maneno ya kishujaa aliyozungumza,
yamezidi kumtia ujasiri wa kusonga mbele katika kudai haki.
Ameona hakuna cha kupoteza
Alisema ujasiri huo umeongezeka kutokana na kuona hakuna cha kupoteza.
“(Ukizungumza
na Lissu unapaswa ujiulize) Juu ya unachofanya kuhakikisha haki
inapatikana, juu ya nafasi yako katika kutetea haki ya Watanzania na
demokrasia kwa ujumla,|” anasema.
“Maana yake nini? Maana yake ni kwamba tunatakiwa kufika mbali zaidi ya alipofika yeye. Nani muoga tena leo.”
“Tuna
imani tukifa leo, wapo watakaohoji kifo chetu, huku waliotuua nao
watakufa kama si leo kesho baada ya kutekeleza mauaji yetu, kila mmoja
atakufa haijalishi kwa kifo cha aina gani, Lissu anatoa mwanga wengine
tunaufuata. ”
Msigwa alitumia msemo wa “kama huna cha kukifia, huna sababu ya kuishi”, kwa hiyo wamepata kitu cha kufia.
Maneno kama hayo yamesemwa na Zitto, ambaye ni kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na mbunge wa Kigoma Mjini.
Zitto na maneno mazito
Zitto
anajulikana kwa mapambano ya hoja na siasa za kistaarabu, lakini katika
siku za karibuni ameonekana kutoa maneno mazito yaliyomfanya aingie
matatani na vyombo vya dola.
“Siku mbili hizi
nilizoenda kumuona Lissu zimeniacha nikiwa na mawazo sana, nimerudi
nchini nikiwa mwenye unyenyekevu zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri
ambao ndugu yangu amenionyesha,” ameandika Zitto katika ukurasa wake wa
Facebook.
“Siyo mara nyingi hapa nchini kusikia
tukiongelea ujasiri, lakini namfikiria Lissu na vile nilivyojisikia
nikiwa pamoja naye Nairobi, najua hivyo ndivyo alivyo.”
Zitto pia amezungumzia hali ya Lissu inavyowafanya watu waongeze ujasiri.
“Ukiona hali ya Lissu, unaumia sana. Kosa lake nini?” anahoji.
“Lengo
la waliompiga ni nini? Kumnyamazisha kabisa? Jawabu kwa hao
waliomshambulia Lissu ni nini? Kuwa kama Lissu. “Hawawezi kutuua wote.
kama kila mmoja akiwa mkali kama Lissu, wauaji hawatafanikiwa kwani
hawawezi kutuua wote.”
Amesema pia kuwa Lissu alimwambia kuwa waendelee alipoishia na akipona ataanzia walipofikia.
“Hivyo
ninamshikia ninamshikia Lissu zamu na naomba kila mwenye uwezo afanye
hivyo ili kulinda uhuru wa kukosoa na uhuru wa mawazo,” ameandika Zitto.
Kiongozi
mwingine aliyepata fursa ya kumuona Lissu ni mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ambaye alisema kama kuna Mtanzania imara,
asiyeogopa na mwenye maono makubwa ni Lissu.
‘Kawaambie nitarudi mzima’
Alisema risasi zote zilizopenya kwenye mwili wa Lissu, zimemtengenezea “uimara maradufu, mara sabini, mara mia moja”.
“Waliodhani
kuwa kumuua Lissu ndiyo kuua harakati za Watanzania za kudai taifa la
haki na linalofuata misingi ya sheria na katiba bora, wamejidanganya,”
anasema Mtatiro.
“Lissu ameniambia ‘Mtatiro nenda
kawaambie kuwa nitarudi nikiwa mzima na tutaendelea na mapambano
maradufu zaidi, faraja muhimu ninayohitaji kutoka kwa Watanzania hivi
sasa ni kuendeleza mapambano ya kudai haki.”
Mtatiro alisema alichojifunza kwa Lissu na kinachompa ujasiri ni kusema ukweli.
“Ukizungumza
naye (Lissu) ni kama anakusuta jinsi alivyo jasiri. Anakusuta kwa maana
yeye yupo tayari kufa au kupambania uhai wake ili aikomboe nchi
kutokana na kila aina ya udhalimu,” alisema Mtatiro.
Mtatiro
alisema ukimuona Lissu kitandani, unamuona mtu ambaye bado ana ari
kubwa ya kuitetea nchi yake pamoja na yote yaliyomkuta.
Alisema hali hiyo inakufanya uwaze mara mbili una kipi cha kupoteza wewe ambaye hujafanywa kitu chochote.
Alisema
hata mkewe ambaye ungetegemea umkute ametetereka, amechanganyikiwa au
ana hofu, lakini anakupokea kwa bashasha na ujasiri wa wazi.
Lissu na marejeo ya sheria
Alisema
ukizungumza na Lissu anatumia muda mwingi kukupitisha kwenye vifungu
vya sheria, michakato ya kudai haki katika mataifa mengine na
kukusisitiza kuwa imara kuendelea kulipigania taifa kwa njia za
kidemokrasia.
“Ukienda kumuona Lissu uzalendo wako,
usimamizi wako wa demokrasia katika nchi kama ulikuwa na mashaka,
ukizungumza naye unajengeka na unapata ujasiri zaidi,” alisema.
Alisema
kupona kwa Lissu kumeongeza hamasa hata miongoni mwa wananchi ambao kwa
vitendo wameonyesha nia ya kutaka kwa kila hali apone.
“Hii
inaonyesha ni kwa namna gani wanaukubali mchango wake, sembuse
mwanasiasa na kiongozi kama mimi. Hili limeniongezea kitu maishani,”
alisema.
Pengine kauli za kijasiri zaidi ni zile
zilizotolewa na Sheikh Ponda, ambaye ni katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Tanzania, ambaye hadi jana alikuwa anashikiliwa na Jeshi la
Polisi kwa mahojiano baada ya kuzungumza na waandishi kuhusu safari yake
ya Nairobi.
Alisema alikwenda Nairobi kwa lengo la
kumfariji na kumtia nguvu Lissu, lakini mbunge huyo ndiye aliyefanya
kazi ya kumpa ujasiri na kumtia nguvu.
“Nimepata ujasiri. Badala ya mimi kumpa matumaini, yeye ndiye aliyenipa matumaini,” alisema Sheikh Ponda.
Alisema
Lissu alimwambia kuwa atarudi hivi karibuni katika harakati zake na
ataanzia alipoishia na kwamba amemuhimiza mshikamano.
Naye
Nyalandu, ambaye ni mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) amekuwa akitoa
kauli tofauti tangu atoke kumuona Lissu jijini Nairobi.
Tabasamu pana
Nyalandu amekuwa akiandika katika akaunti zake za mitandao ya kijamii kuhusu haja ya kuwasaka waliomshambulia Lissu.
Alisema Lissu alikuwa na tabasamu pana alipokuwa akizungumza naye licha ya kuumia.
Nyalandu ni miongoni mwa viongozi waliokwenda kumuoa Lissu siku za awali kabisa tangu alipopigwa risasi mjini Dodoma.
Naye
mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche alisema amepata ujasiri
zaidi kwa sababu anaamini hakuna jambo linaloonyesha uwoga uliokithiri
kama mtu anapofikiria kuua ili amnyamazishe mzungumzaji.
Alisema
kutokana na hilo hakuna cha kuogopa zaidi ya kuzungumza, kwa sababu
inaonyesha anayetakiwa kusikia kinachozungumzwa amekisikia na kimemtisha
ndiyo maana anaamua kuua.
“Haitakuwa na maana kuwa mpinzani halafu ukawa mnafiki kwa kupindisha ukweli. Kusema ukweli kumemgharimu Lissu,” alisema.
“Ili kulipa damu yake iliyomwagika, tuliobaki tunapaswa kusema ukweli.”
SOURCE MWANANCHI.
SOURCE MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment