Thursday 9 November 2017

Askari waliopiga wananchi washtakiwa Bungeni


MBUNGE wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), ameliomba Bunge kuitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi wanaotuhumiwa kutembeza kichapo kwa siku mbili jimboni kwake mwishoni mwa mwezi uliopita.

Aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana alipoomba Mwongozo wa Kiti cha Spika akikiomba pia chombo hicho cha kutunga sheria kiitake serikali ifanye tathmini ya uharibifu wa mali za wananchi kutokana na tukio hilo ili iwafidie.

Akiwasilisha hoja yake hiyo, Waitara alidai kuwa Oktoba 24 askari wa FFU walifunga mitaa wa Mongo la Ndege, Mombasa, Mazizini na Gongo la Mboto na kuwapiga wananchi.

"Wakawapiga watu sana, wakavunjavunja meza za kinamama, wakapiga vijana wa bodaboda," alisema, hiyo haikutosha, Oktoba 25, wakaamkia tena kazi ileile, wanasimamisha magari kutoka hapo magereza, unashushwa unatembezwa kichurachura.

"Tunapozungumza kuna watu wamevunjika miguu, wameporwa fedha zao halafu wakachukua watu kama mia moja wakawasambaza vituo tofauti tofauti.

"Tumeuliza wale watu hawajulikani walipo. OCD anasema hajui, lakini mpaka leo (jana) hakuna kauli ya serikali."

Waitara alikiomba Kiti cha Spika kitoe mwongozo kuhusu suala hilo akidai kuwa kwa sasa hali ni tete jimboni kwake kutokana na uhasama uliopo kati ya wananchi na askari polisi.

"Askari waliokuwa wamepanga kwenye nyumba za wananchi, hapo nyuma walikuwa na mahusiano mazuri, lakini sasa kuna uhasama mkubwa kweli kweli," alisema.

Waitara aliongeza: "Mheshimiwa Mwenyekiti, unisaidie mambo mawili -- kwanza madhara yaliyotokea, tathmini ifanyike, waliopigwa, wakaporwa mali zao, mamalishe wale, wana vikoba wanadaiwa, nani anawafidia? Pili, Wizara yenye dhamana wamechukua hatua gani?"

Katika mwongozo wake, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, aliyekuwa anaongoza kikao cha jana, aliitaka serikali kulifanyia kazi suala hilo na kumpatia majibu mbunge huyo.

0 comments:

Post a Comment