Hali
ya sintofahamu imejitokeza katika jiji la Harare baada ya vifaru
kuonekana vikielekea mjini ambako vilitumika kufunga barabara kubwa za
kuingia na kutoka nje.
Aidha
vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kwamba msafara mkubwa wa
wanajeshi wenye silaha ulizingira kituo cha televisheni kinachomilikiwa
na serikali ZBC. Kadhalika Shirika la Reuters limesema vifaru vinne
vilionekana mitaani.
Baadhi
ya watu walianza kusambaza picha za magari ya kijeshi kwenye mitandao
ya kijamii. Baadhi walisema (mapinduzi) lakini gazeti la Independent la
Uingereza limeshindwa kuthibitisha ukweli wa picha hizo na msafara wa
magari hayo ya kijeshi.
Hata
hivyo, tukio hilo limekuja siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi Jenerali
Constantino Chiwenga kutishia kuingilia kati na akaagiza “kusitishwa”
mara moja ufukuzaji wanachama kutoka chama cha Zanu PF cha Rais Robert
Mugabe kufuatia kufutwa kazi kwa Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa.
Jenerali
Chiwenga akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari
uliohudhuriwa na walau makamanda 90 wa ngazi ya juu kwenye makao makuu
ya jeshi, Jumatatu alisema: "Ufukuzaji huu unaolenga wanachama wa chama
wenye uhusiano na harakati za ukombozi lazima ukome mara moja."
Ripoti
zinasema kwamba jeshi limekuwa likimuunga mkono Mnangagwa kumrithi
Mugabe, 93, lakini mke wa mzee huyo Grace ameibuka na kuwa mshindani
mwenye nafasi kubwa.
Mnangagwa
alifukuzwa serikalini na kwenye chama wiki iliyopita baada ya
kushutumiwa kwamba alikuwa anapanga njama za kumwondoa mamlakani Mugabe.
Mnangagwa amekimbilia uhamishoni.
Waziri
wa Elimu ya Ufundi Jonathan Moyo amemkemea Jenerali Chiwenga lakini
umoja wa vijana wa Zanu PF umesema “uko tayari kufa” ili kuitetea
serikali ya Rais Robert Mugabe.
"Sisi
kama vijana wa Zanu-PF ni simba aliyesimama imara na mwenye sauti, kwa
hiyo hatutalemaa na kukunja mikono yetu wakati vitisho vikitolewa dhidi
ya Mugabe," ilisema taarifa ya Katibu mkuu wa vijana wa Zanu-PF Kudzai
Chipanga.
0 comments:
Post a Comment