Wednesday 29 November 2017

Magari 44 yakamatwa Bandarini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro kuwakamata, Bw. Bahman wa kampuni ya NAS na Wakala wa Kampuni ya Wallmark Bw. Samwel kwa kutaka kutoa bandarini magari makubwa aina ya semi trela 44 bila ya kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu


Pia Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha wa kodi kutoka kwa viongozi wa juu Serikalini.
“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria” amesema.
Hatua hiyo imekuja baada ya Bw. Bahman wa kampuni ya NAS kutaka kupata msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba wamewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.
Waziri Mkuu amefafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa magari hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kwenye kampuni Serin ya nchini Uturuki.
“Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka ambayo inaonyesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani  (bill of lading) inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakin huyu bwana hajafanya hivyo”
Waziri Mkuu amesema kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka hizo ni kinyume cha sheria na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki.
Amesema jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhohofisha mahusiano mazuri iliyopo kati ya Tanzania na Uturuki kwani tayari kampuni hiyo imeshawasilisha malalamiko hayo katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania

0 comments:

Post a Comment