Friday 24 November 2017

Mugabe kupewa kinga maalum


Mugabe atapewa ulinzi pamoja na familia yake nyumbani kwake Zimbabwe. Pia amehakikishiwa kuwa hatashitakiwa kwa makosa anayodaiwa kuyafanya wakati wa utawala wake wa kiimla uliodumu kwa miaka 37
Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robet Mugabe, pamoja na mke wake, Grace Mugabe, wataruhusiwa kuishi nchini humo bila kushitakiwa makosa waliyoyafanya. Hayo yamesemwa na msemaji wa chama tawala ZANU-PF. Wakati huohuo Uingereza imeutaka utawala mpya wa Zimbabwe kuweka wazi nia yao ya kuirejesha nchi katika mkondo wa demokrasia na wa maendeleo.
Msemaji wa chama  tawala nchini Zimbabwe ZANU-PF, Simon Khaya Moyo, ameliambia shirika la habari la DPA kuwa Mugabe angali shujaa wa ukombozi anayeheshimiwa na kwamba alitekeleza mengi ya maendeleo kwa taifa wakati wa utawala wake.
Moyo amesema "Rais anayeondoka anafahamu vyema chuki ya umma dhidi ya mke wake na ghadhabu kutoka pande mbalimbali kuhusiana na jinsi alivyoshughulika na siasa za ZANU-PF. Kwa mantiki hiyo, ilikuwa muhimu kumpa uhakikisho kwamba familia yake yote, akiwemo mkewe, watakuwa salama."
Kinga dhidi ya kushtakiwa
Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe na mkewe Grace Mugabe
Hatua ya kumpa Mugabe kinga imepokelewa vyema na baadhi ya watu, mmoja wao ni mkaazi wa Harare Munyaradzi Makosa: "Ninafikiri ni sawa kwamba rais wa zamani amepewa kinga kwa sababu amefanya mengi ya ukombozi wa nchi na japo alikosea mwisho mwisho, anastahili kinga."
Duru inayofahamu mazungumzo yaliyopelekea Mugabe kujiuzulu, imesema kuwa wamekubaliana kwamba kiongozi huyo atapewa ulinzi pamoja na familia yake nyumbani kwake na amehakikishiwa kuwa hatashitakiwa kwa makosa anayodaiwa kuyafanya wakati wa utawala wake wa kiimla uliodumu kwa miaka 37.

0 comments:

Post a Comment