Serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ambao unaiua rasmi Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kuanzisha shirika jipya la mawasiliano Tanzania ambalo litamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Muswada huo, umewasilishwa bungeni jana Jumanne na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa huku wabunge wakipinga baadhi ya vifungu vya muswada huo.
Akiwasilisha muswada huo, Profesa Mbarawa alisema madhumuni yake ni kuanzisha shirika hilo kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi, kukuza uchumi na kutoa huduma kwa jamii.
Profesa Mbarawa alisema sheria hiyo mpya itaiwezesha TTCL kutekeleza majukumu yake kama shirika la umma la mawasiliano likijulikana kama Tanzania Telecommunication Corporation.
Amesema mambo muhimu ya kuzingatiwa katika muswada huo ni kuwa unakwenda kuifuta TTCL na kuanzisha shirika jipya.
Sheria hiyo ambayo itaumika Tanzania bara na Zanzibar, ilipendekeza muundo wake na mtendaji mkuu na wajumbe watano ambapo upande wa Tanzania Zanzibar utakuwa na mjumbe mmoja.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, inaelekeza kwamba ili mtu awe na sifa ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu ni lazima awe na uzoefu wa miaka nane katika ngazi ya juu ya utawala.
Hata hivyo wabunge waliungana kutaka Zanzibar iwe na wajumbe wawili badala ya mmoja katika bodi ya wakurugenzi na wakataka pia na uzoefu wa mtendaji mkuu uwe miaka mitano badala ya saba.
Mbali na suala la uwakilishi wa Zanzibar, lakini wabunge hao wa CCM na wale wa upinzani, waliungana pia kutaka waziri asiwe na madaraka makubwa ya kuingilia uendeshaji wa shirika hilo.
Wabunge karibu wote waliochangia pamoja kambi rasmi ya upinzani bungeni, wakapendekeza Zanzibar ipewe nafasi mbili kati ya tano badala ya moja, ili kuleta sura halisi ya muungano.
Hata hivyo, Naibu Spika Dk Tulia Ackson alitahadharisha mwelekeo wa mjadala huo akisema hilo si shirika la kwanza la muungano, hivyo wasije wakaanzisha utaratibu mpya kwenye mashirika.
0 comments:
Post a Comment