Thursday 14 December 2017

Mjue James Dandu 'Cool james massive'


James Dandu au kwa jina lingine Cool James Massive; 'CJ Massive ' alizaliwa Julai 5, 1970, Mwanza nchini Tanzania. Alisoma shule ya Msingi Kurasini na baada ya hapo, yeye, mama yake na ndugu zake walihamia jijini Stockholm, Sweden alikoishi kwa kipindi kirefu.

ALIVYOINGIA KWENYE GEMU
James Dandu aliingia rasmi kwenye sanaa ya muziki mwaka 1988 akiwa jijini Stockholm ambapo alitoa singo kadhaa zikiwa katika staili ya Euro-House. Mwaka 1992 aliachia albamu yake ya kwanza ambayo hata hivyo haikupata mafanikio makubwa. Mwaka 1993 , aliungana na msanii mwingine kutoka Afrika Mashariki, Andrew Muturi na kuunda kundi lililokwenda kwa jina la "SwahiliNation". Wasanii wengine wawili wakajiunga kwenye kundi hilo.

Baadaye, James Dandu alijitoa kwenye kundi hilo na kuungana na Mkongomani, Jose Masena 'Black Teacher' na kutoa albamu mbili zilizowatambulisha vyema sehemu mbalimbali; Undercover Lover (1992) na Zooming You (1995 ) iliyokuwa na wimbo ulioitwa Dr . Feel Good. Wakapata mafanikio makubwa na kuingiza pesa ya maana.

AREJEA BONGO KWA KISHINDO

Kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa na mwenzake, Black Teacher , Mtoto wa Dandu aliamua kurudisha majeshi nyumbani kwa lengo la kuja kuibua na kuinua vipaji Tanzania na Afrika Mashariki kwajumla. Aliporudi Tanzania alikuja na staili mpya ya uimbaji wa nyimbo za taratibu ( R & B ) ambao haukuwa umezoeleka sana kwa kipindi hicho. Akajipatia umaarufu mkubwa ndani ya kipindi kifupi.

Hakuishia hapo, aliendelea kuingiza ubunifu katika kazi zake akawa anachanganya R &B ya kisasa, Rhumba na Ndombolo (staili iliyokuwa maarufu sana nchini Zaire kipindi hicho). Akatoa albamu nyingine kama Soft Like a Pillow(1997) , Bi Harusi (1998) na Sukuma Land (2002).

Miongoni mwa ngoma ambazo mpaka leo zikipigwa lazima watu watulie ni Sina Makosa ambayo aliurudia wimbo wenye jina hilohilo uliopigwa na Les Wanyika kutoka Kenya. Ngoma hii ilimtambulisha kinoma Afrika Mashariki yote hususan nchini Kenya.

Pia alifanya remix ya wimbo wa Mamu akiwa na mkali Madilu System ambao ama kwa hakika ulibamba mbaya!

TUZO ZA KILI

Mwaka 1999, James Dandu aliamua kuanzisha tuzo alizoziita "Tanzania Music Awards" ambazo hivi sasa zinajulikana kama Kili Music Awards baada ya kuanza kudhaminiwa na bia ya Kilimanjaro. James Dandu ndiye aliyefanikisha usajili wa tuzo hizo kwa kushirikiana na Basata chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni (kipindi hicho).

KIFO CHAKE

Mtoto wa Dandu alifariki Agosti 27, 2002 kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Makumbusho jijini Dar es Salaam nyota yake ikiwa inang'ara kinoma na kuzua simanzi kubwa miongoni mwa mashabiki wake hususan wanawake ambao walikuwa mashabiki wake wakubwa. Akaenda kuzikwa nyumbani kwao, Mwanza.

Wakati anakufa, alikuwa bado hajamaliza kurekodi kazi zake mpya katika Studio ya Master Jay. Aliacha watoto wawili wakiwa bado wadogo pamoja na mjane, Devotha.

0 comments:

Post a Comment