Saturday 30 December 2017

Mpango wa kuapishwa 'rais wa wananchi' Kenya upo pale pale




Kiongozi wa chama cha Wiper nchini Kenya Kalonzo Musyoka Alhamisi alitangaza kuwa ataapishwa na Raila Odinga iwapo Rais Uhuru Kenyatta hatakubali kufanya mazungumzo na upinzani.
Kalonzo amesema mipango ya kuapishwa iko katika maandalizi na suala hilo haliwezi kuzuiliwa muda wa kuwa Rais anashikilia msimamo wake dhidi ya kuwepo mazungumzo ambayo yangeweza kutatua dhulma zilizojitokeza wakati wa uchaguzi.
Makamu wa Rais mstaafu amedai kuwa kuapishwa kwa Raila kama rais wa watu na yeye mwenyewe kama makamu wake umejikita katika sheria na uhalali wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 ambapo amedai kuwa Muungano wa upinzani Nasa ulishinda.
Kalonzo amesema haikubaliki kabisa kwa Rais kulinganisha juhudi zao za kuwepo na mazungumzo sawa na kufanyika uchaguzi wa urais 2022 na kuwa hawatarudi nyuma.
“Hivi Rais hana moyo? Moyo wangu unavuja damu. Mimi na kaka yangu Raila tutaendelea na sherehe za kuapishwa kama rais na makamu wake wa wananchi iwapo hatozingatia wito wetu wa kuwepo mazungumzo ili kuondoa dhulma ya uchaguzi katika nchi hii. Hatuwezi kusimamisha kuapishwa kwetu,” alitangaza uamuzi huo.
Mahakama ya Juu nchini Kenya ilibatilisha ushindi wa Uhuru katika uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8 kufuatia Raila kupinga matokeo hayo na kutaka marudio ya uchaguzi yafanyike Oktoba 26, ambapo Rais alishinda baada ya viongozi waNasa kususia uchaguzi huo.

0 comments:

Post a Comment