Wednesday 24 January 2018

Filamu ya Kenya yatajwa kuwania tuzo za Oscar


Filamu kuhusu shambulizi la kigaidi la Alshabaab nchini Kenya ambapo watu 28 waliuawa ndani ya basi eneo la Mandera mwaka 2014 imeteuliwa kushindania tuzo maarufu za Oscar mwaka huu.
Filamu hiyo ilikuwa imeshinda tuzo za Oscar kitengo cha wanafunzi mwaka jana na kuwa filamu ya kwanza kutoka Kenya kushinda tuzo hiyo.
Filamu hiyo ya Watu Wote imeorodheshwa kushindania kitengo cha Filamu Bora Fupi: Matukio Halisi.
Itashindana na filamu nyingine nne ambazo ni "Dekalb Elementary", "The Eleven O'Clock", "My Nephew Emmett" na "The Silent Child".
Filamu hiyo inayoeleza hadithi ya Kenya, kuhusu Wakenya na inashirikisha waigizaji wa Kenya, inasimulia shambulio hilo la mwaka 2014 kaskazini mwa Kenya, ambapo maudhui ya uadui wa kidini kati ya Wakristo na Waislamu yanaangaziwa.
Ni mara ya kwanza ambapo filamu ya kenya imeteuliwa kuwania tuzo ya Oscars.

Katika shambulizi hilo, Waislamu walikataa kujitenga na Wakristo walipoamriwa kufanya hivyo na magaidi wa Alshabaab kutoka Somalia.
"Ni hadithi kuhusu Kenya na undugu wa Wakenya, na inaonyesha njia mwafaka ya kukabiliana na ugaidi kote Ulimwenguni".
Filamu hiyo iliyoundwa kwa ushirikiano wa wanafunzi wa Ujerumani na watengenezaji filamu wa Kenya inalenga kuwakumbuka mashujaa wa shambulizi hilo.
Filamu inaonyeshwa Kenya kwa mara ya kwanza leo jijini Nairobi.
Kwa miaka kadha, Kenya ilikuwa ikishambuliwa na wanamgambo wa al-Shabaab.
Mwaka 2015, wanafunzi zaidi ya 147 waliuwawa na Al-Shabab katika chuo kikuu cha Garissa kaskazini mwa Kenya.

0 comments:

Post a Comment