Tuesday 30 January 2018

JESSE LINGARD NA NDOTO YA KUTISHA


    Na Raphael Mwenda.
         Roy Benavidez mmoja kati ya watu wenye roho ngumu zaidi duniani yaani ni kama aligoma kufa vile, Benavidez alikua ni master sergeant katika jeshi la Marekani, alipelekwa katika vita ya Vietnam na huko alifanikiwa kupata vidonda 37 katika mwili wake vilivyo sababishwa na majeraha ya risasi alizopigwa alivunjwa taya na pia upofu wa muda mchache baada ya macho kuvia damu na mwisho alichomwa kisu na utumbo kuning'inia nje. Kufikia hapo alipelekwa mochwari kwakua watu wa huduma ya kwanza walithibitisha kuwa kafariki. Wakati anawekwa kwenye mfumo wa kuhifadhia maiti aliamka na kumtemea daktari mate usoni na kumwambia sifi leo wala kesho nirudishie utumbo wangu ndani nirudi vitani.
                  Kwenye maisha inahitajika roho ngumu na mbaya kama ya sergeant Benavidez ili kufikia malengo. Kwa vizazi na vizazi watu wengi wamekua wakikata tamaa na kushindwa kufikia malengo kutokana na kuanguka na kushindwa kunyanyuka kutokana na sababu mbalimbali wengine wameogopa hata kujaribu kushindwa kutokana na uoga na kuogopa watu watasema nini juu yao lakini daima maisha ni kupambana na kutokata tamaa mpaka pumzi ya mwisho.
               Baada ya miaka mingi ya tukio lile hatimae nimepata kumshuhudia binadamu mwingine mwenye roho kama ya sergeant Benavidez. Binadamu huyu aitwae Jesse Lingard yeye si mtu wa majeshi bali ni msakata kabumbu hadithi ya maisha yake inavutia na inatia nguvu katika kupambana na maisha. Uliitajika moyo wa chuma na imani Kali kama jua la mchana kwa Jesse Lingard kufika pale alipo leo. Si kila binadamu na mwanasoka angeweza kukifikia kile alichofikia leo Lingard.
              Akiwa na umri wa miaka 25 Lingard anapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake ulimwenguni anapata nafasi ya kuaminika na maelfu ya mashabiki wa soka duniani haikua kazi rahisi bali kujituma na kutokata tamaa katika vipindi vigumu vya maisha ndio silaha, ndio kwanini usikate tamaa katika timu kubwa kama Manchester United ambayo kila siku inahusishwa na majina makubwa, kwanini usitamani kuondoka ikiwa nafasi unayocheza yupo mtu mwingine mwenye uwezo mkubwa sana.
              Lakini Lingard aliamini alikubali kujifunza na nafasi ilipokuja aliipokea kwa mikono yote miwili na kuitendea haki. Jesse Lingard aliipa Manchester United kombe la FA mwaka 2016 lakini nani alimpa sifa zake na kuusifu uwezo wake? Sifa zote alipewa Chris Smalling kwa rafu yake kwa Yannick Bolasie aliekua akienda kufunga, Lingard akabaki kuwa shujaa asiepewa sifa yake stahiki, Lingard aliipatia tena Manchester United kombe la ngao ya jamii lakini sifa zilikwenda kwa Jose Mourinho na Zlatan Ibrahimovic nani alimfikiria Lingard hakuna.
               Najaribu kuwaza kama Ibrahim Ajibu aliondoka pale simba kwasababu ya uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni au kutopewa ile heshima yake aliyostahili najiuliza leo Jesse angekuwa wapi? Najaribu kutafakari yule mfanyakazi wa ofisini anaefanya kazi kwa bidii lakini hapandishwi mshahara nae anaishia kulalamika je angekua ni Jesse angefanyaje? Vijana wengi mtaani wanalalamika maisha ni magumu hela hakuna na kazi pia hakuna ndio ni kweli lakini je kuna hela ama kazi inayomfuata mtu nyumbani?
             Baada ya lawama nyingi kuwa hajakua anawaza kucheza muziki bila kuwaza kazi yake uwanjani anapenda maisha ya starehe yote haya yalikua maneno juu ya Jesse lakini daima aliamini katika jitihada zake na uwezo wake pia aliamini maneno ya biblia pia yasemayo Mungu hakupi ukitakacho bali hukupa unachostahili kwa wakati sahihi. Ndio naamin roho ilikua ikimuuma sana Jesse alipokua akimuona Anthony Martial anacheza kila siku huku yeye akiwa katika benchi roho yake ilizidi kumuuma pale Marcus Rashford alipopandishwa kutoka timu ya watoto na kuja kucheza kila siku huku yeye akiwa katika benchi.
               Na katika maumivu yake hayo hayo bado aliongezewa Henrikh Mkhitaryan, Andres Pereirra alikataa kuishi katika ndoto hii mapema aliamua kukimbilia Valencia Josh Harrop aliogopa kulala pale old trafford kuhofia kuota ndoto mbaya kama hii Matty Willock aliamua kwenda vittese ilimradi tu asiote ndoto mbaya kama hii. Ndio ni ndoto mbaya sana hakuna mchezaji anaependa kukaa benchi hakuna mchezaji asiependa kulipwa mshahara mzuri lakini ili upate vyote hivi ni lazima upambane kwa jasho na damu.
           Jesse Lingard alikua tayari katika hili hakuona tabu kuamini kuwa ipo siku ndoto zake alizokua akiota tangu utotoni za kua ipo siku moja atacheza kikosi cha kwanza cha Manchester United kila siku hakujali kuona Angel Di maria yupo pale Radamel Falcao pia hakuogopa kuona Adnan Januzaj akishindwa kutimiza ndoto hii hakuhofia kumuona Mkhitaryan akikaa benchi alikua mkimya Juan Mata alivyoendelea kuicheza nafasi yake yote haya aliyatumia kama changamoto za maisha katika kufikia malengo na hatimae ameyafikia.
                Vuta shuka vizuri Jesse Lingard lala salama uendelee kuota ndoto hii ya kutisha moyo na roho yako katika ugumu ule wa sergeant Benavidez ama hakika unastahili pongezi imekua darasa tosha kwa vijana na binadamu wote wanaokata tamaa katika maisha kwa kuwaaminisha ipo siku moja maisha hubadilika na kuwa upande wako hakuna mtu asiependa kufanikiwa katika maisha lakini hakuna njia rahisi pia ya mafanikio katika mafanikio ni lazima kuumia ili kupata kile unachostahili, sidhani kama ni binadamu sote tungependa kuota ndoto hii pamoja na Jesse Lingard. Lala vizuri Jesse Lingard bado ni usiku wa manane ila pakikucha tukutane carrington kuendelea na mapambano katika maisha.

0 comments:

Post a Comment