Tuesday 22 May 2018

UN yaomba dola milioni 80 kusaidia waathirika wa mafuriko nchini Somalia


Idara zinazosimamia haki za binadamu za serikali ya Somalia pamoja na Shirika la umoja wa mataifa linashughulikia haki za binadamu zimetoa ombi la fedha dola za kimarekani milioni 80 ili kuwasidia waathirika wa mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa jumapili, fedha hizo zitasaidia kutoa msaada wa haraka kwa watu walioathirika na mafuriko ya hivi karibuni katika maeneo ya katikati na kusini mwa nchi yaliyotokana na mvua ambayo haijawahi kunyesha yapata miongo mitatu iliyopita.

Mafuriko hayo yamesababisha vifo, idadi kubwa ya watu kuyahama makazi yao, na uharibifu wa miundo mbinu pamoja na mashamba yenye mazao.

Mratibu Mkazi wa shirika la Umoja wa mataifa la haki za binadamu nchini Somalia, Peter de Clercq, ameeleza kuwa zaidi ya watu 750,000 wanakadiriwa kuwa wameathirika na mafuriko hayo na zaidi ya 229,000 wamehama makazi yao. Hivyo fedha hizo milioni 80 ni kiasi kinachotakiwa na mashirika hayo ili kutoa msaada wa haraka.

0 comments:

Post a Comment