Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu nchini (HESLB) imewatoa hofu wanafunzi
waliokosa mikopo kwakuwa ipo katika hatua za mwisho kutoa majina ya
awamu ya tatu.
Kauli hiyo imekuja ikiwa leo ni siku ya mwisho iliyotolewa na Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ya kuitaka bodi
hiyo kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye sifa anapewa mkopo.
Akizungumza na gazeti hili leo Novemba 3,Meneja Mawasiliano wa bodi
hiyo, Omega Ngole amesema agizo hilo linaendelea kutekelezwa na kwamba
hadi kufikia kesho kila mwanafunzi mwenye sifa atapata mkopo.
Amesema kwa wale watakaokosa mkopo wanaweza kukata rufaa kupitia bodi hiyo ili kupitia upya taarifa zao.
“Maelekezo hayo yote yanatekelezwa na tutakamilisha leo na tutatoa taarifa ya kuhusu utekelezaji wake wiki ijayo,” amesema
Katika mwaka wa masomo wa 2017/18 Serikali imetenga bajeti ya Sh427
bilioni kwaajili ya mikopo ambapo wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza
watanufaika na fungu hilo.
Hadi sasa Jumla ya wanafunzi 21,677 maombi yao yamekubaliwa ikiwa ni
awamu mbili zilizotolewa na bodi hiyo ambapo awamu ya kwanza ilitoa
majina 10,196 na ya pili 11,481.
Meneja huyo amesema kwa wale waliodahiliwa kwenye vyuo walivyothibitisha
kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) tayari fedha zimeanza kutumwa kwenye
vyuo husika.
“Mwanafunzi akipangiwa mkopo halafu asipoliridhika, akaona uhitaji wake
ni mkubwa kuliko kiwango alichokipata kuna nafasi ya kukata rufaa ambayo
itaanza wiki ijayo,”amesema.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na gazeti hili walieleza kuwa hatua ya
kuchelewa kwa majina imeibua wasiwasi huku wakikosa kufanya udahili kwa
muda uliopangwa.
Mwanafunzi Athuman Mohamed, aliyechaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha
Dar es Saalam ,alisema ameanza kukata tamaa baada ya jina lake kutooneka
kwenye awamu zote mbili huku mzazi akieleza hana uwezo wa kugharamia.
“Mimi mpaka muda huu nimekata tama mchana huu nimewasiliana na mzazi kaniambia uwezo huo yeye hana,”
“Kwa sasa nasubiri awamu ya tatu nione kama ntapata kama nikikosa
ntaangalia kama naweza kuandika barua ya kuahirisha mwaka au niache moja
kwa moja,”amesema
Naye, Ebrania Sanga alisema ameshindwa kufanya udahili kutokana na kutegemea mkopo wa bodi.
“Sina uwezo kabisa hatma yangu ipo kwenye mkopo hapa nilikuja na nauli
tu na ndiyo kwanza inamalizika kesho nikishindwa kusoma basi nitafanya
shughili nyingine,”amesema
Wakati wanafunzi hao wakilalama kukosa mikopo, Justine Joshua (Udsm)
alisema bado ana matumaini kwani hata akikosa mkopo wa bodi ataomba
kwenye taasisi ya Msaada wa Kijamii (TSSF).
Taasisi hiyo imewataka wanafunzi waliokosa mkopo kwa mwaka wa masomo 2017/18 kutuma maombi kwaajili ya kupata ufadhili.
Hatahivyo bodi hiyo imesema licha ya kuendelea na mchakato huo kuna
baadhi ya wanafunzi wamekosa sifa kutokana na uzembe ikiwamo kutojaza
taarifa sahihi.
SOURCE MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment