Tuesday 28 November 2017

Duru yakutafuta usuluhisho Syria yaanza Geneva

Duru ya nane ya mazungumzo ya kutafuta amani Syria imeanza Geneva lakini tangazo la dakika za mwisho la Serikali ya Syria kuwa huenda isitume wajumbe ni pigo kwa juhudi za kutafuta suluhisho kwa mzozo wa Syria.

Duru hii ya mazungumzo ilionekana kama fursa ya mwisho ya Umoja wa Mataifa kusogesha mbele juhudi za kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu, kuwaacha mamilioni bila ya makazi na kuharibu vibaya miundo mbinu Syria.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura amesisitiza kuna haja ya kupatikana kwa dharura suluhisho la kisiasa. Upande wa upinzani kwa mara ya kwanza unatuma ujumbe wa pamoja katika mazungumzo hayo.
Serikali haijatuma wajumbe
Hapo Jumatatu, de Mistura aliliambia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa serikali ya Rais Bashar al Assad bado haijathibitisha kutuma ujumbe katika mazungumzo hayo.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura akizungumza Geneva Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura
Hayo yanajiri huku Viongozi wa Marekani na Ufaransa wakisisitiza kuwa mazungumzo ya kutafuta amani Syria yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa ndiyo njia pekee ya kuamua mustakabali wa siku za usoni wa Syria.
Ikulu ya Rais wa Marekani imesema Rais Donald Trump na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron walizungumza kwa njia ya simu na kukubaliana kuwa mazungumzo yanayoanza leo mjini Geneva kuhusu Syria ndiyo njia pekee halali ya kufikia suluhisho la kisiasa Syria.

0 comments:

Post a Comment