Friday 17 November 2017

Mugabe 'Mimi ndio Rais wa Zimbabwe'


Rais Robert Mugabe ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutojiuzulu wadhifa wake, wakati wa mkutano kati yake na majenerali wa ngazi ya juu wa kijeshi ambao wamechukua udhibiti wa Zimbabwe.
President Robert Mugabe poses with General Constantino Chiwenga at State House in Harare (Reuters/Zimpapers/J. Nyadzayo)

Mazungumzo hayo yamefanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Harare, baada ya wanajeshi kuzuia barabara kuu, kuchukua udhibiti wa kituo cha televisheni ya taifa pamoja na kumuweka katika kizuizi cha nyumbani Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 93, pamoja na mkewe Grace na mawaziri kadhaa.
Kituo hicho cha televisheni kilimuonyesha Mugabe akiwa amevalia koti la rangi ya buluu iliyokoa pamoja na suruali ya kijivu akiwa amesimama pamoja na Mkuu wa Majeshi, Constantino Chiwenga aliyekuwa amevalia sare za kijeshi. Mugabe ambaye ameitawala Zimbabwe tangu ilivyopata uhuru wake mwaka 1980 kutoka kwa Uingereza, amekataa kuachia madaraka, baada ya kukutana pia na wajumbe kutoka Afrika Kusini.

Kiongozi wa upinzani wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai amemtaka Mugabe kuondoka madarakani. Tsvangirai waziri mkuu wa zamani na mpinzani wa muda mrefu wa Mugabe amewaambia waandishi habari mjini Harare kwamba kiongozi huyo anapaswa kujiuzulu kwa maslahi ya wananchi. Amesema kipindi cha mpito kitahitajika ili kuhakikisha kuna utulivu.Taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo ya kuutatua mzozo wa Zimbabwe, yanaendelea. Awali, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma aliliambia bunge la nchi yake mjini Cape Town, kwamba ni mapema mno kuchukua uamuzi thabiti kutokana na hali ya kisiasa iliyopo, ambayo muda si mrefu itajulikana wazi.
Mwanasiasa mwigine wa Zimbabwe anayeheshimikwa kimataifa, Tendai Biti amesema njia inabidi ipatikane ili kudumisha utulivu. Biti aliyewahi kuwa waziri wa fedha wakati wa serikali ya muungano baada ya uchaguzi wa mwaka 2008, amesema mpango wa amani unahitajika na kwamba malalamiko yaliyosababisha hali hiyo yanapaswa kujadiliwa.

0 comments:

Post a Comment