Umoja wa Ulaya (EU)umechukua msimamo wakutatanisha katika kukabiliana na misimamo ya rais wa Marekani, Donald Trump, ya kupinga mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kwa jina la JCPOA ingawa hata hivyo umoja huo unajaribu kuonesha kuwa haukubaliani na Marekani katika mambo yote.
Pamoja na Umoja wa Ulaya kujaribu kuonesha kuwa haukubaliani na Marekani katika kila kitu, lakini hadi hivi sasa haiwezekani kusema kwa yakini kwamba nchi zote za Ulaya zina msimamo mmoja kuhusu suala hilo.
Ushahidi unaoensha kuwa, baadhi ya nchi za Ulaya kama vile Ufaransa zinayaangalia mapatano ya nyuklia ya JCPOA katika upande wa manufaa yao binafsi ya kiuchumi na hilo ndilo linalozifanya nchi za Ulaya ziyatetee makubaliano hayo. Viongozi wa Ufaransa ambao tab'an ndio waliowekeana na Iran mikataba mingi zaidi ya kiuchumi baada ya kuanza kutekelezwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA imekuwa mara kwa mara ikitoa matamshi yenye utata kuhusu misimamo ya Marekani na kudai kuwa hata Paris nayo ina wasiwasi na nguvu za makombora za Iran.
Matamshi ya hivi karibuni kabisa ya Ufaransa ni yale yaliyotolewa na waziri wake wa mambo ya nje ambaye amedai kuwa ana wasiwasi na uwezo wa makombora wa Iran. Kwa upande wake, Rais Emanuel Macron wa Ufaransa hivi karibuni alitoa matamshi kama yale ya Marekani ya kutaka kujadiliwa pia mradi wa makombora wa Iran na nafasi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na alifika mbali hadi kusema kuwa vikwazo dhidi ya mradi wa makombora wa Iran ni moja ya njia zinazoweza kufikiriwa za kukabiliana na Tehran.
Hata juzi tu, shirika la habari la Reuters lilimnukuu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa akisema kuwa Paris inauhesabu mradi wa makombora wa Iran kuwa ni kikwazo cha kupatikana utulivu na amani katika eneo la Mashariki ya Kati na ina wasiwasi na suala hilo.
Kabla ya hapo, Rais Emanuel Macron wa Ufaransa aliwahi kudai kuwa Paris na Marekani hazina msimamo mmoja kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Pamoja na hayo hivi sasa anasema kuwa hakuna matatizo kufanyika mabadiliko kidogo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Ni jambo lisilo na shaka kwamba nchi zote zikiwemo za Umoja wa Ulaya zinafikiria tu maslahi yao. Hivyo si jambo la kushangaza kuiona Ufaransa ikibadilisha badilisha misimamo yake kulingana na maslahi yake binafsi. Hivi sasa Ufaransa imelipa umuhimu mkubwa suala la kuziuzia silaha nchi za Kiarabu zinazopakana na Ghuba ya Uajemi, hivyo jambo hilo linaathiri moja kwa moja misimamo ya Paris. Lakini pia Ufaransa inaona inafaidika sana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA hivyo haitaki kupoteza maslahi yake hayo. Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa mtazamo huo wa Ufaransa wa kutaka kuwa na msimamo mmoja na Marekani na wakati huo huo kulinda maslahi yake ndani ya JCPOA ni wa upande mmoja. Msimamo huo wa viongozi wa hivi sasa wa Ufaransa si tu unaonekana hautekelezeki, lakini pia hauwezi kupata uungaji mkono hata ndani ya Umoja wa Ulaya wenyewe.
Kwa kweli kati ya nchi za Ulaya, Ufaransa ni moja ya nchi zisizo na mwamana kabisa. Uhusiano wa Ufaransa na Iran umekumbwa na misukosuko mingi katika miaka ya hivi karibuni. Hata wakati wa mazungumzo ya nyuklia yaliyoishia kwenye mapatano ya JCPOA, Ufaransa ilikuwa moja ya nchi zilizokuwa zikikwamisha sana mambo. Wakati wa vikwazo pia, Paris ilikuwa mstari wa mbele kupalilia vikwazo hivyo ikiwa ni pamoja na kuvunja mikataba iliyowekeana na Tehran. Si hayo tu, lakini pia Ufaransa mara kwa mara imekuwa mwenyeji wa vikao vya kijikundi cha kigaidi cha MKO chenye historia ya kuwaua shahidi Wairani 17 elfu.
Amma lililo wazi ni kwamba, Iran itaendelea kufanya juhudi za kuyalinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA, lakini kamwe haitakuwa tayari kulinda mapatano hayo iwapo yatapoteza manufaa yake kwa pande husika.
Katika miongozo yake ya hivi karibuni, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kusimama kidete kukabiliana na vitendo vya serikali ya Marekani ikiwa ni pamoja na kuyavunja waziwazi mapatano ya JCPOA na zisikubali kuwa na sauti moja na Wamarekani katika masuala kama vile uwezo wa kiulinzi wa Iran na ushawishi wa Tehran katika eneo hili kwani kamwe Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kukubaliana na madola yenye sauti moja na mabeberu wa Marekani.
0 comments:
Post a Comment