Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 06 Novemba, 2017 ameanza ziara ya kikazi ya siku 4 katika Mkoa wa
Kagera.
Akiwa
njiani Kutoka Chato Mkoani Geita alikokuwa mapumzikoni kuelekea Bukoba
Mjini Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Muleba na Kemondo,
Bukoba Vijijini na kuwahakikishia kuwa Serikali itasaini mkataba na
kampuni ya kutoka Jamhuri ya Korea kati ya mwezi Desemba mwaka huu na
Januari mwakani kwa ajili ya kuanza kuunda meli mpya katika ziwa
Victoria itakayokuwa na uwezo wa kubeba idadi kubwa ya abiria na mzigo
mkubwa zaidi ikilinganishwa na meli zilizopo
“Tunaunda
meli ya kisasa itakayobeba abiria wengi na mizigo mingi, na pia
tutakarabati meli zilizopo za MV Victoria na MV Butiama, tunataka pamoja
na kujenga barabara, tuhakikishe kuna meli za uhakika ili muweze
kusafiri na kusafirisha mazao yenu kwenda kwenye masoko” amesema Rais
Magufuli.
Kuhusu
ufugaji Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera
kuhakikisha mifugo yote inawekwa alama kwa mujibu wa sheria, ili
kurahisisha utambuzi wa mifugo inayoingizwa nchini kutoka nchi jirani na
pia kudhibiti ruzuku inayotolewa na Serikali kwa dawa za mifugo ya hapa
nchini.
“Tanzania
sio shamba la kuchungia mifugo ya nchi jirani, ndio maana tumeamua
kukamata mifugo na kuchukua hatua kwa mujibu wa kisheria, na hata huko
kwenye nchi jirani wakishika mifugo ya kutoka Tanzania wachukue hatua za
kisheria za nchi hizo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Hata
hivyo amewataka wananchi wa Kagera kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi
ikiwemo hifadhi ya Burigi na ameagiza viongozi wa Wilaya ya Muleba
kufuatilia madai ya wananchi juu ya kuuzwa kwa ardhi ya kijiji
kulikosababisha wananchi kukosa maeneo ya kulima na kulisha mifugo yao.
“Na
kuna watu waliouziwa ranchi na Serikali, watu hao hawajaziendeleza
ranchi hizo na badala yake wanawakodisha wananchi, wafuatilieni na
mkiona hawajaziendeleza nyang’anyeni muwape wananchi wazitumie kwa
ufugaji, lakini pia hakikisheni wananchi hawavamii maeneo ya hifadhi
yaliyotengwa” ameongeza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa na Wilaya za Mkoa wa
Kagera kuwachukulia hatua maafisa wote wa halmashauri ambao bado
wanawatoza ushuru wakulima wanaosafirisha mazao yaliyo chini ya tani
moja kwa kuwa tayari Serikali imeshaamua kuondoa adha hiyo na
kuwawezesha wakulima wadogo kunufaika na kilimo chao.
Mchana wa leo (06 Novemba, 2017) Mhe. Rais Magufuli atafungua mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Bukoba
06 Novemba, 2017
0 comments:
Post a Comment