Monday 12 February 2018

Bi Ellen anyakua Tuzo ya Mo Ibrahim


Rais wa zamani wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf ameshinda tuzo ya mwaka ya Mo Ibrahim kwa Uongozi wa Afrika - ambayo hupewa viongozi wa Afrika ambao wameonekana kuwa na utawala mzuri.
Ellen Johnson Sirleaf amekuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kushika nafasi ya Urais mwaka 2006 na kumaliza muda wake mwezi uliopita baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.
Kamati ya Utendaji ya tuzo ya Mo Ibrahim imesema Ellen Johnson Sirleaf ameonesha uongozi wa kipekee katika kukabiliana na changamoto zisizowahi kutokea katika awamu zake mbili za uongozi alipokuwa Rais wa Liberia.
Wakati aliposhinda uchaguzi wa Rais nchini humo mwaka 2005, nchi hiyo ilikuwa imegawanyika kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka kadhaa na tuzo hiyo ya amani ilikuwa ni kwa ajili ya kumpongeza kusaidia kuiimarisha nchi hiyo.
Wakosoaji wake wamekuwa wakimkosoa kwa kuwa na upendeleo, kutokana na kuwachagua watoto wake katika nafasi za ngazi za juu na pia wanadai kuwa hakuchukua hatua za kutosha kupambana na rushwa.
Kamati yab utendaji ya Mo Ibrahimu imearifu kwamba inafahamu mapungufu yake, lakini imeamua kwamba anastahili kupata tuzo ya dola za kimarekani milioni 5.

0 comments:

Post a Comment