Wednesday 28 February 2018

MUCHAS GRACIAS GUARDIOLA.


Na Raphael Mwenda.
         Maisha ni bahati,ndio ni bahati inayotakiwa kuitolea jasho hasa kuipata japo si kila aipatae kaitolea jasho la hasha,mafanikio ni malipo ya upambanaji na kujituma kwa mtu husika mwanasoka Christiano Ronaldo amewahisema 'watu wanalalamika kuhusu fedha nyingi ninazolipwa lakini wanasahau nguvu ninazotumia kila uchwao ili kulipwa pesa hizi wamesahau maisha niliyokulia mpaka leo kupata hiki' ndio Christiano ni mmoja kati ya wanasoka wenye historia ya kuvutia hasa kutoka utotoni mpaka mafanikio aliyonayo hii leo.
         Nchini Hispania kuna jimbo linaitwa Catalonia alimaarufu kwa lugha yetu 'katalunya' watu wa jimbo hili wanasifika kuwa na kiburi dharau tamaa ya kuwa juu na kujipenda wao tu, sikushangaa niliposikia Catalonia inataka kujitenga na Hispania nao wao na nchi yao. Katika jimbo hili ndipo alipozaliwa Josep "Pep" Guardiola Sala bosi wa pale Etihad. Huyu jamaa anakiburi anaijua jeuri haswaa na mpira kichwani upo kweli kweli. Alikulia La Masia akademia ya Barcelona katika ardhi ya kwao Catalonia ameichezea Barcelona katika timu ya wakubwa akitokea katika mfumo wa kusapoti vijana ambao ni mfumo mama wa klabu hiyo ulioleta matunda ya akina Leonel Messi, Anders Iniesta, Xavi Hernandez, Serge Roberto na wengineo wengi.
           Baada ya kuichezea Barcelona kwa mafanikio makubwa alipotundika daluga Pep alipewa jukumu la kuifundisha Barcelona ya vijana kule alipotokea 'La Masia' mnamo mwaka 2007 hakukaa sana hapo kwani mnamo mwaka 2008 Pep alikabidhiwa timu ya wakubwa baada ya kocha mkuu Frank Rijkaard kuachia ngazi. Hapa ndipo dunia ilipomtambua hasa Josep 'Pep' Guardiola ni nani. Hakuna shabiki wa soka asiejua umahiri wa Samuel Etoo katika kutupia kambani vipi kuhusu ubora wa Ronaldinho usisahau kiwango cha Yaya Toure achilia mbali cheche za Deco lakini kichwani na katika mtazamo wa Pep hawa walikua wachezaji wa kawaida sana ambao aliona hawastahili kuichezea Barcelona.
            Lionel Messi akawa chambo ya Ronaldinho, Sergio Busquet akamtega kwa Yaya Toure Deco akapewa Xavi Hernandez, Etoo akaachiwa apambane na Pedro Rodriguez achilia mbali Andres Iniesta aliekua akipata nafasi, hawa wote ni wacatalonia wenzake ambao wametokea kule kule alipotoka yeye na wamekulia La Masia pale pale alipokulia yeye achilia mbali Leonel Messi mwanavita kutoka Argentina mwenye ubora wa Ak-47 hawa wote Pep aliumia kuwaona katika benchi hakupenda kabisa wakae nje alifanya kila awezalo mpaka walicheza bahati nzuri kwake alipowapa nafasi hawakumuangusha.
              Miaka imeenda na nyakati zimebadilika maisha yale ya Leonel Messi wa bure hakuna tena maisha ya Gerald Pique wa bei chee watu wamekwisha sahau labda swahiba wake mzee Wenger bado anayo. Mnamo mwaka 2016 Pep alikabidhiwa kikosi cha Manchester city kilichosheheni wazee wengi kwa kiburi na jeuri yake alianza kwa kumtema goli kipa namba moja wa city na timu ya taifa ya Uingereza Joe Hart na akaleta wake. Katika msimu ule city iliondoka mikono mitupu hata maji ya kunywa haikuomba Pep kwa Mara ya kwanza katika historia yake alimaliza msimu bila kikombe walau kimoja si yeye pekee bali hata mashabiki wa City pia waliumia sana kwani walitegemea makubwa sana kutoka kwake.
              Pep aliinamisha kichwa chini kwa aibu huzuni huku akitunga sheria na kutafuta dawa ya kutibu magonjwa sugu ya timu za uingereza na ulaya kwa ujumla. Kwa kiburi hakuuza mchezaji asiemuhitaji bali alimuacha aende bure kabisa bila kujali ubora wa mchezaji husika hatimae akavunja benki kwa kumnunua Ederson Morales kutoka Benfica na kuwa kipa ghali zaidi duniani akaenda Tottenham akamchukua Kyle Walker kwa hela za kutupa akaenda kule Ufaransa akawavamia Monaco akambeba Benjamin Mendy kwa hela ya madafu hakuishia hapo akawavamia Real Madrid akamchukua Danilo kuja kuongeza nguvu kwa wachezaji hawa tu niamini unanunua kikosi kizima cha Arsenal ya mzee Wenger na chenji itabaki.
               Ukuta wa Berlin ukawekwa pale Etihad roho ngumu akavishwa Fernandinho katikati ya uwanja baraka akabarikiwa Kelvin De Bruyne na David Silva kufanya kila watakacho uwanjani kwanini timu isishinde? Aguero anafunga Sterling anafunga Leroy Sane anafunga wakishindwa basi waliobaki watafunga timu nzima inafunga kwanini watu wasipigwe  sita? Pasi za uhakika silaha yao kasi ya kuutafuta mpira pale waupotezapo kwanini mpinzani usichanganyikiwe?
               Muchas Gracias (Asante sana) Pep kwa kukubali kuwa zama za kina Leonel Messi katika akademia hakuna tena maisha ya akina Gerald Pique kwa bei ya mkate hakuna tena mpira wa sasa ni biashara na umekubali kuacha tamaduni za kikatalonia na kwenda sambamba na mpira wa kisasa asanteh sana Pep.

0 comments:

Post a Comment