Saturday 5 May 2018

BBC,VOA vyafungiwa Burundi


   




Serikali ya Burundi imetangaza kuvifungia vituo vya kimataifa vya utangazaji vya BBC na VOA kurusha matangazo nchini humo kwa miezi 6 kuanzia Mei 7 mwaka huu.

Katika taarifa iliyotolewa na Rais wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo, Karenga Ramadhani sababu ya kufungiwa huko ni kufanya mahojiano na watu walioiasi Burundi wanaoishi ughaibuni na kuyarusha nchini humo kitu ambacho ni kinyume na Sheria za mawasiliano na ni uchochezi.

Sambamba na adhabu hiyo, vituo vingine vitatu vya redio RFI, Isanganiro na CCIB FM vimepigwa onyo kali huku gazeti Le Renouveau la nchini humo likifungiwa miezi mitatu kwa kuandika makala zenye uchochezi zilizolenga kuikosoa serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.

Hii inafanyika ikiwa ni siku 1 baada ya maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani na takribani wiki 2 kabla ya wananchi wa Burundi kupiga kura ya maoni ambayo itaongeza ukomo wa muda wa Urais.

Kama zoezi hilo likifanikiwa Rais Nkurunziza atakuwa na nafasi ya kuiongoza Burundi hadi 2034 kwa vipindi viwili vya miaka 7 kila kimoja kuanzia 2020.

Rais huyo aliingia madarakani 2005 baada ya kuisha kwa vita nchini humo na kusainiwa kwa makubaliano ya amani. Mwaka 2015 aligombea kwa kipindi cha 3 na kuvunja makubaliano hayo hali iliyopelekea vifo vya mamia ya watu.

Imeripotiwa kuwa vikundi vya upinzani nchini humo vimejawa na uoga wakati wakipanga kupinga zoezi hilo.

0 comments:

Post a Comment