Mahakama
ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha/ Arumeru imewatia
hatiani waliokuwa wafanyakazi 6 wa Benki ya Exim tawi la Arusha na
kuwatupa jela jumla ya miaka 27.
Watuhumiwa
hao walishitakiwa kwa makosa 318, ikiwa ni pamoja na kughushi, kuharibu
nyaraka, utakatishaji fedha haramu na wizi wa dola za kimarekani
521,000 mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Wakati
hukumu inatolewa, mmoja wa waliotiwa hatiani amempoteza mtoto katika
ajali ya gari, wakati kijana huyo akisafiri kuwahi kusikiliza hukumu ya
mama yake.
Kijana huyo ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), David Chijana.
Akisoma
hukumu hiyo kwa zaidi ya saa 5 kuanzia saa 4.30 asubuhi hadi saa 9.07
alasiri, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Deusdedit Kamugisha aliwataja
aliowatia hatiani ni pamoja na mshitakiwa namba mbili Liliani Mgeye
(33), Daudi Nhosha (39), Doroth Chijana (50), Genes Massawe (32), Christopher Lyimo (34) na Deusdedit Chacha (35).
Aidha,
mahakama hiyo imewaachia huru watuhumiwa saba kwa kile ilichoeleza kuwa
upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha makosa yao.
Hakimu
Kamugisha aliwataja walioachiwa huru na mahakama baada ya upande wa
Jamhuri kushindwa kuthibitisha katika ushahidi wao kuwa watuhumiwa hao
walitenda makosa hayo kuwa ni pamoja na mshitakiwa wa kwanza katika kesi
hiyo ambaye alikuwa Meneja Mkuu wa Benki ya Exim (T) Ltd tawi la
Arusha, Bimel Gondaili. Wengine ni pamoja na Livingstone Mwakihaba (37)
maarufu kwa jina la Stone, Joyce Kimaro (36), Evance Kashebo (40),
Tutufye Agrey (32), Joseph Neki(30) na mfanyabiashara Gervas Lubuva(54).
Adhabu
Hakimu
Kamugisha alisema katika hukumu yake kwa mujibu wa sheria ya
utakatishaji fedha haramu, kifungo cha chini ni miaka mitano na kuharibu
nyaraka na kughushi ni miaka 14.
Hata hivyo kwa mujibu wa hukumu iliyosomwa, mtuhumiwa Mgeye, Chijana na Chacha ambao wamekutwa na makosa yote mawili, watatumikia kifungo cha miaka mitano jela bila ya faini kila mmoja.
Aidha
alisema watuhumiwa wengine waliokutwa na makosa ya kughushi nyaraka na
kuharibu nyaraka ambao ni pamoja na Nhosha, Massawe na Lyimo
wamehukumiwa kwenda jela miaka minne kila mmoja kwa kosa hilo.
Awali
kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Mwendesha mashitaka wa serikali,
Felix Kwetukia aliitaka mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya waliotiwa
hatiani kwa kuitaka mahakama kufuata sheria ya kifungo cha miaka mitano
jela ama faini ya kiwango cha chini cha shilingi milioni 100 kila mmoja.
Kwetukia
alisema serikali imeibiwa fedha za umma zilizotakiwa kufanya maendeleo
kwa jamii, lakini wahusika walifanya wizi na kujitajirisha wao bila ya
woga hivyo adhabu kali inahitajika.
Kutokana
na hoja hiyo mawakili wa utetezi wakiongozwa na Philipo Mushi waliiomba
mahakama kutoa nafuu ya hukumu kwa waliotiwa hatiani kwani ni kosa lao
la kwanza na wamejutia kosa hilo na pia wanafamilia inayowategemea.
Ajali ya gari
Chijana
ambaye ni miongoni mwa watu wawili waliokutwa na mauti baada ya gari
walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Mark X Saloon yenye rangi nyeusi,
ikiwa na namba za usajili T796 DFG inadaiwa ndiye alikuwa dereva
akitokea Moshi mkoani Kilimanjaro, kuelekea Arusha jana asubuhi.
Imeelezwa
kuwa Chijana alipata ajali katika barabara kubwa ya Moshi-Arusha,
makutano ya Momella, Usa-River ambayo ni sehemu ya Wilaya ya Arumeru.
Ilielezwa
na watoa habari kuwa mmiliki wa gari hilo, David Chijana, kabla ya
kupata ajali alionywa na askari wa usalama barabarani na kupigwa faini
ya shilingi 30,000 kutokana na mwendo kasi na pia taa zake za breki kuwa
na matatizo.
Imeelezwa
kuwa alilipa faini na kuendelea na safari kabla ya kupata ajali
iliyomtoa uhai yeye na mwenzake ambaye bado kutambulika, kwa mujibu wa
Polisi.
Imeelezwa
kuwa gari hilo likiwa katika mwendo kasi lilipofika katika makutano ya
Momella, dereva alijaribu kupita gari lingine ndipo alipokutana uso kwa
uso na basi, lililokuwa likisafiri kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam na
kujaribu kukwepa ajali.
Kwa
mujibu wa mashuhuda, Chijana alifanikiwa kulitoa gari katika hali ya
kugongana uso kwa uso na basi hilo lakini gari lilimshinda likaserereka
na kugonga mti mkubwa.
Kwa
sababu ya spidi na kujigonga kwenye mti kwa kishindo, gari hilo
lilirushwa juu na kupinduka, tairi juu na kuwaua watu wote wawili
waliokuwamo humo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha kutokea kwa
ajali hiyo na kuongeza kuwa atatoa taarifa rasmi pamoja na jina la
marehemu wa pili baada ya upelelezi kukamilika.
Inadaiwa pia, mmoja kati ya waliokufa ambaye ni mfanyakazi wa TPA alikuwa anatarajia kufunga ndoa hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment