Tuesday 28 November 2017

Uhuru Kenyatta aahidi mabadiliko makubwa Kenya

 

Nitaangazia umoja wa taifa na huduma ya afya

Kenyatta amesema ana malengo mawili muhula wake wa mwisho. Kwanza kuimarisha uwiano na umoja miongoni mwa Wakenya.
Amesema ameanza kuwasiliana na viongozi wote na kueleza nia yake ya kuendeleza umoja.
Amesema lengo la pili ni kuhakikisha huduma ya afya inawafikia Wakenya 100%.
Katika miaka mitano ijayo, nitahakikisha Wakenya 13 milioni wanafaidi kupitia huduma ya NHIF. NHIF itafanyiwa mageuzi pamoja na sheria za kusimamia kampuni za bima za kibinafsi.
Amesema atafanikisha mpango wa kumiliki nyumba na makazi.
"Kwa miaka mitano ijayo serikali yangu itaangazia kuhakikisha watu wengine 500,000 wanajipatia nyumba," amesema.

Uwanja wa Jacaranda ni kama mahame

Uwanja wa Jacaranda, Embakasi jijini Nairobi ambapo muungano wa upinzani Kenya Nasa ulipanga kufanya mkutano umebaki kama mahame.
Polisi wamezingira milango yote ya kuingia uwanja huo.

Kenyatta: Najivunia ugatuzi na miundo mbinu

Rais amesema anajivunia mambo manne ambayo serikali yake ilitimiza miaka minne iliyopita. Mwanzo ugatuzi wa mamlaka na rasilimali, pili ni msingi wa ukuaji wa kiuchumi na kibiashara. Pia ujenzi wa reli ya kisasa na kusambazwa kwa umeme mashinani.
"Tatu tumewekeza katika mageuzi yanayoboresha utoaji wa huduma ya afya. Aidha, upanuzi wa miundo mbinu ya hospitali na Bima ya Afya ya Taifa (NHIF).
"Nne, tumefanyia mageuzi mfumo wetu wa elimu. Kurejesha imani katika mfumo wa mitihani na kuimarisha tena taasisi za elimu."

Kenyatta: Tunaweza kujenga Kenya tunayojivunia

Rais amesema kwa pamoja, bila kujali tofauti za kidini na za kijamii, Wakenya wanaweza kujenga Kenya imara na inayostawi kwa pamoja.
Lakini amesema lazima waacha kuangazia makovu ya kale, na pia kwa kufuata sheria.
"Sheria lazima itawale. Inafaa kuwa kimbilio kwa kila Mkenya na hakuna yeyote anafaa kuvunja sheria au kwenda nje ya mfumo wa sheria bila kujali ukubwa wa malalamiko yako.
"Niwakumbushe, Mahakama ya Nje ilipotutaka tujitee, tulitii. Mahakama ya Juu ya Kenya ilipofuta uchaguzi wetu, hata baada ya kushindwa, baada ya kuambiwa utaratibu ulikuwa muhimu kuliko kula, tuliheshimu uamuzi huo.
"Serikali yangu imedhihirisha kujitolea kuheshimu sheria. Tunatarajia raia wote wengine wafanye hivyo."
"Katiba yetu imeunda mihimili mitatu huru ya serikali...lazima kila mtu afanye kazi yake."
"Matamanio ya binadamu wakati mwingine huzidi kipimo, na yasipodhibitiwa, yanaweza kulibomoa taifa. Ili kuishi pamoja, lazima watu wakubaliane kufuata sheria fulani. Kenya ni nchi ya watu zaidi ya 40 milioni. Tumeishi pamoja ishara kwamba hata tukitofautiana huwa twajua jinsi ya kuungana tena.
"Matatizo mengi hutokea tunapokosa kufuata sheria hizi. Miezi minne iliyopita, tumefanyia majaribio sheria hizi. IEBC, Mahakama, Idara za Usalama. Hizi zote zimefanyiwa majaribio na siasa, na zimesalia imara.
"Uamuzi usipoenda unavyotaka, unaheshimu, hiyo ni demokrasia.
"Tumejifunza kwamba taasisi zetu ni kakamavu kuliko tulivyodhani awali."
"Hatufai kubomoa taasisi zetu kila wakati zikikosa kutoa matokeo tunayotaka."

Kenyatta: Leo ni mwisho wa shughuli yetu ya uchaguzi

Kenyatta amesema leo ni siku ya 123 tangu kufanyika kwa uchaguzi Agosti 8 na kusema shughuli ya uchaguzi sasa imefikia kikomo, na akasisitiza tena.
Anaonekana kupuuzilia mbali upinzani ambao umekuwa ukisisitiza kwamba uchaguzi wa 26 Oktoba haukuwa huru na wa haki na kwamba uchaguzi mpya unafaa kuandaliwa.

Kenyatta: Nitakuwa rais wa Wakenya wote

Bw Kenyatta amesema aliwasikiliza kwa makini wapinzani wake uchaguzini na kwamba atatekeleza baadhi ya mawazo na mapendekezo yao.
"Naahidi kulinda ndoto za wote na maono ya wote, walionipigia kura na waliokosa kunipigia kura. Nitakuwa rais wa wote. Na nitajitolea muda wangu na nguvu kujenga madaraja, kuunganisha Wakenya na kuleta ustawi."

Kenyatta aishukuru mahakama kwa maamuzi huru

Bw Kenyatta amesema Mungu aliyajibu maombi na kwamba atawafikisha Wakenya mbali.
Ameishukuru tume ya uchaguzi kwa kuendesha uchaguzi, chini ya shinikizo nyingi.
Ameisifu Mahakama na kusema ilifanya maamuzi yake kwa uhuru.

Kenyatta: Asanteni sana Wakenya

Rais Kenyatta sasa anahutubu na ameanza kwa kuwashukuru waliohudhuria.
Ameomba kuhutubia kwa Kiingereza kwa sababu ya wageni.
"Hamjambo Wakenya?" ameanza, na kusema amefika kutuma hongera, na kuwapongeza Wakenya kwa kudumisha amani.
"Nawaomba Wakenya wote wakumbuke mambo matatu manne muhimu. Jambo la kwanza ni amani. Jambo la pili ni ustawi wa jamii. Jambo la tatu maendeleo. Na jambo la nne siasa."
"Msifikirie siasa peke yake mkasahau yale mengine matatu.

Lungu: Kama marafiki tulikuwa na wasiwasi

Rais wa Zambia Edgar Lungu amealikwa kuhutubu kwa niaba ya viongozi wengine wa mataifa.
"Wakenya Mpo? Asante sana," ndivyo alivyoanza.
Amewapongeza Wakenya.
"Tuna furaha sana kwamba shughuli hii imekamilika, tunawahimiza tu mrejee kazini. Kama marafiki, tulikuwa na wasiwasi kwamba shughuli hii ilichukua muda mrefu. Tunatumai mtalifikiria hilo siku za usoni.
Ali Bongo Ondimba wa Gabon pia amealikwa kuhutubu na kusema anajivunia sana leo kuwa Mwafrika.
"Nyinyi watu wa Kenya mmetufanya kujionea fahari sana," amesema.
"Wananchi wa Kenya hamjambo? Tumekuja hapa kusema hongera, hongera sana," huyo naye ni Paul Kagame wa Rwanda.
Kumalizia ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Yoweri Museveni.

Ruto: Tumekusanyika pia kusherehekea demokrasia

Bw Ruto amesema leo pia Wakenya wamekusanyika kusherehekea demokrasia ya Kenya, baada ya uchaguzi.
"Kwamba tuna uwezo wa kuamua mustakabali wetu, kuwachagua viongozi wetu na mwelekeo wa taifa letu la Kenya."
Amesema uchaguzi wa wakati huu ulikuwa na mambo mawili wakuu, tofauti na ule wa 2013.
Kwamba serikali iliungana chini ya chama cha Jubilee na upinzani uliungana chini ya Nasa.

0 comments:

Post a Comment