Thursday 7 December 2017

Naibu Waziri Mkuu wa Urusi afungiwa na Olimpiki kutojihusisha na michezo maisha yake yote

Kamati ya Olimpiki duniani IOC imeifungia Urusi kutoshiriki michuano ijayo ya Olimpiki Pyeongchang 2018, sambamba na kumfungia Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Vitaly Mutko kutojihusisha na michezo hiyo maisha yake yote. Vitaly Mutko ni waziri wa zamani wa michezo nchini Urusi aliyetumikia kuanzia mwaka 2008 hadi 2006 alipopata nafasi ya kuwa Naibu Waziri Mkuu.

Mutko amekumbana na rungu hilo baada ya ripoti ya uchunguzi kumkuta na hatia ya kukwamisha zoezi la mamlaka ya kuzuia dawa za kuongeza nguvu michezoni (WADA) la kuwachunguza wanamichezo wa Urusi kwenye Olimpiki ya 2014 Sochi. Mwingine aliyekutana na kifungo cha maisha kutojihusisha na michezo ya Olimpiki ni Yuri Nagornykh, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa michezo akimsaidia Mutko wakati makosa hayo ya kukwamisha uchunguzi yakifanyika. Naye rais wa shirikisho la Olimpiki nchini Urusi (ROC) Alexander Zhukov ameondolewa uanachama wa IOC, wakati bosi wa zamani wa kamati ya Olimpiki ya Sochi 2014 Dmitry Chernyshenko ameondolewa kwenye kamati ya maandalizi ya Olimpiki ya Beijing 2022.

0 comments:

Post a Comment