Sunday 21 January 2018

Hoteli ya Intercontinental Mjini Kabul yavamiwa na magaidi

Wanajeshi wa Afghanistan, wamekuwa wakipigana ghorofa baada ya ghorofa, ili kuchukua udhibiti wa hoteli moja ya kifahari katika mji mkuu Kabul, baada ya kuvamiwa na wapiganaji waliokuwa na silaha nzito nzito.

Yamkini watu 20 wanahofiwa kuwawa baada ya hoteli maarufu ya Intercontinental mjini Kabul, Afghanistan kushambuliwa na magaidi.

Msemaji wa Wizara ya usalama wa ndani nchini humo amesema kwamba, washambuliaji wawili kati ya wavamizi wanne, tayari wameuwawa.
Washambuliaji hao walivamia Hoteli ya Intercontinental jana Jumamosi jioni, na kuanza kuwamiminia risasi wageni na wafanyikazi pamoja na kurusha magruneti.

Msemaji wa Wizara ya usalama wa ndani nchini humo, Nasrat Rahimi, ameiambia BBC kuwa, walinda usalama wamechukua udhibiti wa ghorofa ya kwanza ya kifahari ya hoteli hiyo, lakini baadhi ya washambuliaji bado wangali katika orofa zingine hotelini.
Taarifa zingine zinasema kwamba, wakati wa uvamizi huo, hoteli hiyo ilikuwa inaandaa kongamano la Teknolojia ya mawasiliani (IT) iliyokuwa inahudhuriwa na maafisa wa mikoa.
Shahidi mmoja ameiambia shirika la habari la Reuters kuwa, washambuliaji hao wanawazuilia baadhi ya watu kama mateka.
Shambulio hilo linatokea siku kadhaa baada ya ubalozi wa Marekani mjini Kabul, kutoa tahadhari ya uwezekano wa kutokea shambulio la kigaidi lililolenga mahoteli kadhaa mjini Kabul.
Kufikia sasa haijabainika ni watu wangapi wameuwawa au kujeruhiwa, lakini taarifa ambazo bado hazijathibitishwa na BBC, zinaasema kuwa watu 15 wameuwawa.
Sehemu moja ya jumba la Hoteli hiyo inateketea, huku makabiliano makali ya risasi yakiendelea.
Jumba la Hoteli hiyo ya Intercontinental, linachukuliwa kama nembo ya mji mkuu Kabul.
Hoteli hiyo ilishambuliwa na kundi la wapiganaji wa Taliban, miaka 7 iliyopita.

0 comments:

Post a Comment