Saturday 20 January 2018

Marekani yazitaja Urusi na China kuwa kitisho kikubwa zaidi kwake


Marekani imeziainisha China na Urusi kuwa kitisho kikubwa zaidi kwake, katika mkakati wa usalama wa taifa. Moscow imeitaja sera hiyo ya Washington kuwa ya "kibepari," huku China ikisema ni "fikra ya enzi za vita baridi."
Akiwasilisha mkakati huo mpya, ambao unabainisha vipaumbele vya wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon kwa miaka kadhaa ijayo, waziri wa ulinzi Jim Mattis ameziita China na Urusi kuwa "madola yanayobadili itikadi ya kisiasa" yanayotafuta kuunda ulimwengu unaowiana na ruwaza zao za utawala wa mkono wa chuma."
Mkakati wa ulinzi wa taifa, unawakilisha ishara ya karibuni ya dhamira ya utawala wa rais Donald Trump kushughulikia changamoto kutoka Urusi na China, na wakati huo akishinikiza kuboresha uhusiano na Moscow na Beijing ili kuidhibiti Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia.
"Tutaendelea kutekeleza kampeni dhidi ya ugaidi ambayo tunashiriki wakati huu, lakini ushindani wa kuimarisha nguvu yetu, na siyo ugaidi, ndiyo kipaumbele cha usalama wetu wa taifa," Mattis alisema katika hotuba wakati akiwasilisha waraka wa mkakati huo, wa kwanza wa aina yake tangu alau mwaka 2014.
Unaweka vipaumbele kwa wizara ya ulinzi ambavyo vinatarajiwa kuakisiwa katika maombi ya matumizi ya ulinzi katika siku za usoni. Pentagon ilitoa toleo la kurasa 11 la waraka huo, ambalo halikutoa ufafanuzi juu ya mabadiliko kuelekea kukabiliana na China na Urusi yatakavyotekelezwa.
USA Verteidigungsminister James Mattis (picture-alliance/AP Photo/J. Martin)
Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis
Mkakati wa makabiliano
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, akizungumza kupitia mkalimani katika mkutano wa waandishi habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, alisema Marekani ilikuwa inatumia mkakati wa makabiliano.
"Inasikitisha kwamba badala ya kuwa na majadiliano ya kawaida, badala ya kutumia msingi wa sheria ya kimataifa, Marekani inajitahidi kudhihirisha uongozi wao kupitia mikakati na dhana za ukabilianaji," alisema Lavrov na kuongeza kuwa Urusi iko tyari kwa mazungumzo na majadiliano kuhusu kanuni za kijeshi.
Ubalozi wa China nchini Marekani ilikosoa mkakati huo, ukisema Beijing inataka "ushikirano wa kimataifa" na siyo "udhibiti wa dunia." "Iwapo baadhi ya watu wanaiangalia dunia kupitia vita baridi, basi hatma yao ni kuangalia tu migogoro na makabiliano," alisema msemaji wa ubalozi huo katika taarifa.
Elbridge Colby, naibu katibu msaidizi anaeshughulikia mikakati na ujenzi wa jeshi, alisema wakati wa mkutano na maripota kwamba Urusi ilikuwa fidhuli zaidi katika utumiaji wa nguvu yake ya kijeshi kuliko China.
Urusi iliitwa kimabavu rasi ya Cremea kutoka kwa Ukraine mwaka 2014, na ikaingilia kijeshi nchini Syria kumsaidia mshirika wake, rais wa Syria Bashar al Assad. Lakini bado Moscow ilikuwa ikizuwiwa na rasilimali zake kiuchumi, alisema Colby.
China kwa upande mwingine ilielezwa kama inayopanda juu kiuchumi na kijeshi. China imeanzisha mkakati wa kuboresha jeshi lake, ambao Colby anasema ulikuwa "uingiliaji mkubwa wa maslahi yetu."

0 comments:

Post a Comment