Friday, 5 January 2018

Mtu mmoja kati ya watano wanaofanyiwa upasuaji anakabiliwa na matatizo baadae.


Hatari ya kufariki dunia kutokana na upasuaji wa kitabibu barani Afrika ni zaidi ya mara mbili ya wastani wa Kimataifa, hii ni kulingana na ripoti inayoangazia matatizo ya kiafya barani Afrika.
Utafiti huo umesema kuwa katika hali ya kawaida, wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji barani Afrika hawachukuliwi kuwa katika hatari ikilinganishwa na wenzao kwengineko, kwa vile wengi wao wanakuwa vijana na huwa wanafanyiwa upasuaji mdogo tu.
Lakini watafiti wamegundua kwamba karibu mtu mmoja katika kila watu watano wanaofanyiwa upasuaji barani humo anakabiliwa na matatizo baadae. Aidha, kulingana na ripoti ya wataalmu hao, hatari inayoambatana na upasuaji uliopangwa mapema, yaani ambao sio wa hali ya dharura, iko katika kiwango cha asilimia moja barani Afrika, huku athari hiyo katika wastani wa kimataifa ikiwa asilimia 0.5.
Uchunguzi huo uliochapishwa katika jarida la afya la The Lancet unaelezwa kuwa uchunguzi mkubwa na wa ndani zaidi juu ya upasuaji barani Afrika, uliowaleta pamoja zaidi ya watafiti 30, walioangalia data kutoka hospitali 247 katika nchi 25 barani humo, lengo lao kuu likiwa kufuatilia operesheni 10,885 zilizofanyiwa wagonjwa, thuluthi moja ya hizo zikiwa operesheni za kina mama waliojifungua kwa njia ya upasuaji.
Uchunguzi huo pia ulijumuisha maelezo zaidi kuhusu matatizo yaliyojitokeza, idadi ya vitanda vya kulazia wagonjwa, vyumba na vifaa vya kufanyia operesheni hizo na kupata habari muhimu juu ya miundo mbinu ya hospitali.
Zaidi ya wagonjwa wanne kwa kila wagonjwa watano ambao visa vyao vilichunguzwa, wangeweza kuaminiwa kuwa na hatari ndogo kwa kuzingatia kwanba wengi bado ni vijana walio katika umri wa wastani wa miaka 38, lakini matatizo yaliyotokana maambukizi kufuatia upasuaji yaliwakumba asilimia 18.2 ya wagonjwa wote na takriban mgonjwa mmoja kati ya 10 aliyekuwa mamatatizo hayo aliaga dunia.
Ufuatiliaji wa wagonjwa baada ya upasuaji ni muhimu ili kupunguza vifo vinavyotokea baada ya upasuaji.
Hata hivyo mtafiti mkuu Bruce Biccard, ambaye ni professa katika hospitali ya Groote Schuur iliyoko mjini Cape Town, Afrika Kusini alielekeza kidole cha lawama katika kipindi cha baada ya upasuaji ambapo asilimia 95 ya vifo hivyo hutokea.
Profesa anasema vifo hivi vingeweza kuepukika iwapo kungelikuwepo na ufuatiliaji wa wagonjwa waliokuwa na matatizo. Amesema matokeo ya baada ya uchaguzi yataendelea kuwa mabaya barani Afrika hadi tatizo la vifaa na mazingira salama ya kufanyia kazi litakaposhughulikiwa.
Aidha uchunguzi huo umebaini kuwepo asilimia 0.7 ya madaktari wa upasuaji wa uzazi na wataalamu wa kuwatia ganzi wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji,  kwa kila wagonjwa 100,000 barani Afrika, idadi ambayo ni ya chini mno ya viwango vilivyopendekezwa ya wataalamu, ambavyo ni wataalamu 20-40 kwa wagonjwa 100,000.
Mataifa yaliyofanyiwa uchunguzi ni pamoja na Algeria, Libyana na Misri, lakini haukujumuisha baadhi ya mataifa masikini barani Afrika kama vile Burkina Faso, Liberia na Sudan, au hata taifa linalokumbwa na vita la Somalia. Hospitali ndogo ndogo zilizoko vijijini pia hazikufanyiwa uchunguzi.
SOURCE DW SWAHILI

0 comments:

Post a Comment