Friday 9 February 2018

MUACHE AENDE. AAH! KWANINI ALIONDOKA?


Na Raphael Mwenda.
          Binadamu tumeumbwa na hulka mbalimbali,lakini binadamu tuliowengi haturidhiki. Inaaminika binadamu wa kwanza ulimwenguni aliitwa Adam ambae alishii katika bustani ya Eden iliyokuwa na kila aina ya wanyama na matunda ambavyo Mungu muumba alimpa Adam uwezo wa kuvitawala na kuviamrisha pia, pamoja na yote lakini Adam hakuridhika alihitaji mtu wa kufanana nae. Kwa manung'uniko ya upweke ule Adam aliletewa Eve. Katika bustani ya Eden Adam na Eve waliruhusiwa kula matunda ya aina yote isipokua ya mti ule wa katikati. Lakini mwisho wa yote Eve alikula tunda lile na kumpatia Adam nae pia akalila. Tusiizungumzie sana biblia.
          Vizazi na vizazi kuanzia Adam mpaka hii leo binadamu haturidhiki. Jumatatu ya tarehe 5 mwezi wa pili mwaka huu 2018 majira ya usiku nilikua nikiangalia mechi kati ya Chelsea na Watford katika ubora wao ilikua ni mechi nzuri iliyovutia kutazama lakini ghafla mambo yalibadilika baada ya Tiemoue Bakayoko kupewa kadi nyekundu niliwasikia mashabiki wa Chelsea wakilalama na kumtupia kila aina ya matusi na kudai hawajui kwanini Antonio Conte alimnunua na kumuuza Nemanja Matic, kichwani nikajiuliza si hawa waliokua wakisema muache Matic aende united sisi tuna Bakayoko.
           Nakumbuka kuna mtu amewahi kuniambia Bakayoko ni hatari sana katika viungo wale wa UEFA msimu uliopita na yeye yupo Nemanja tumewaibia Man united hela zao kwanza kazeeka. Najiuliza kwamba Bakayoko nae amezeeka? Au amekuaje kwa maana Chelsea ina kiungo mkabaji Ngolo Kante na Bakayoko ni kiungo mshambuliaji anaepewa majukumu ya kumsaidia kazi Kante kitu kinachomshinda.
             Si mashabiki wa Chelsea tu majuzi juzi tu niliwasikia mashabiki wa Arsenal pia wakisema muache Alexis Sanchez aende tu tayari tuna 'assist king' Henrikh Mkhtaryan mashabiki wa united pia waliaza kulalama kwanini Mikh aliachiwa aondoke mbona ana kiwango kizuri cha kuchezea katika timu yao na kusahau mchango aliowapa Alexis katika mechi zao zote tatu walizocheza wamesahau kuwa Mikh amecheza mechi nyingi za united bila kutoa mchango mzuri sababu ya mfumo wa timu kumkataa.
               Lionel Messi alilalamika kwanini viongozi wa Barcelona walimruhusu Neymar Jr kuondoka pale camp nou akidai Neymar Jr alikua na mchango mkubwa sana katika timu yao ndio hilo ni jambo lisilopingika lakini ghafla Lionel Messi yule yule anaibuka tena na kusema bora Neymar Jr aliondoka katika timu yao kwani sasa wanacheza vizuri kuliko alivyokuwepo hapa unabaki na maswali mengi kuliko majibu.
                Mwaka 2009 mashabiki wa Man united waligawanyika wapo waliosema bora Christiano Ronaldo ameondoka katika timu yao kwani alikua amekwishajiona ni mkubwa kuliko timu pale Old Trafford na wapo waliotambua mchango wa Ronaldo na kulaani kuondoka kwake lakini wakaja kuwa pamoja na kutaka kuiaminisha dunia Antonio Valencia ni Ronaldo mpya hahaha.
                  Muache aende Isco anacheza vizuri sana Marco Asensio nae anakuja kwa kasi tumemuongeza na Dani Ceballos pia, haya ni baadhi ya maneno ya mashabiki wa Real Madrid hawakuumizwa na kuondoka kwa James Rodriguez wakiamini waliopo ni sahihi zaidi hivyo hakuna pengo lake katika timu baada ya msimu wao kuwa hovyo wanadai James angewaongezea kitu kwenye kikosi chao na wasingekua wanacheza hivi unabaki kujiuliza Isco hayupo Asensio je au Dani Ceballos  hajatua kwenye timu yao? Ni mashabiki hawa hawa waliodai muache Alvaro Morata aende tu Chelsea wao wana Karim Benzema hata Christiano Ronaldo pia anaweza kucheza eneo lile kwa ufasaha leo hii wanadai Alvaro Morata angefanya vizuri sana katika timu yao.
               Watuachie timu yetu aliondoka mfalme Thiery Henry akaondoka nahodha Cesc Fabrigas atakua yeye Robin Van Persie muache aende tu yalikua ni maneno rahisi sana kutamka lakini magumu katika utekelezaji hasa pale Van Persie alipoisaidia united kutwaa taji la ishirini huku akiibuka mfungaji bora kwa mara ya pili mfululizo.
                 Waache waende tu watacheza wapi Lampard katika ubora wake lakini mwisho wa umri wake wa soka willian katika ubora Oscar hakamatiki Eden Hazard anafunga na kutoa pasi za mwisho anavyojisikia Ramirez anakimbia uwanja mzima bila kuchoka atacheza wapi Kelvin De Bruyne utamuweka wapi Juan Mata achilia mbali Mohammed Salah na Juan Cuadrado waache tu waende walijigamba mashabiki wa Chelsea lakini baada ya Kelvin De Bruyne kuanza kutupia magoli muhimu na kuwa mchezaji muhimu pale Etihad wanaanza kuulizana kwanini tulimuacha aende zake usiwazungumzie Mo Salah na Juan Mata.
                Katika maisha ninge huja baada ya tukio na ni vyema kujiuliza mara kadhaa kabla ya maamuzi fulani ili kuondoa manung'uniko baada ya tukio husika. Adam baada ya tukio lile alimlaumu mwenyezi Mungu kwa kumletea Eve na kusahau kua aliufurahia sana ujio wake na alimuhitaji sana. Conte anabeba lawama za kumleta Bakayoko Chelsea Mourinho anabeba lawama za kumpeleka Mikh Arsenal Zizzou analaumiwa kwa kuwaacha James na Morata waondoke Mourinho anachukiwa kwa kuwaacha De Bruyne na Salah waondoke huu ndio utamu wa soka na mwisho wa yote maisha lazima yaendelee.

0 comments:

Post a Comment