Tuesday 7 November 2017

Wakamatwa kwa kesi ya kifo cha mtuhumiwa wizi wa simu


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, iliyopewa mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji, imewaona washtakiwa Rashidi Rwambo na Mwanahamisi Shabani wana kesi ya kujibu dhidi ya mauaji ya Saidi Mketo.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Geni Dudu, aliyepewa kibali cha kusikiliza kesi za mauaji mahakamani hapo.

Alisema baada ya kusikiliza ushahi
di wa mashahidi watano wa upande wa Jamhuri bila kuacha shaka mahakama yake imewaona wana kesi ya kujibu.

"Mahakama hii imewaona washtakiwa wana kesi ya kujibu baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi watano wa Jamhuri," alisema Hakimu Dudu.

Kabla ya uamuzi huo, shahidi wa tano, Konstebo Godwin alidai kuwa  Aprili 22, 2012 alikuwa mpelelezi wa zamu katika kituo cha polisi Kibiti.

Alidai kuwa saa 2:30 usiku lilifika kundi la watu kati ya 45 na 50, huku wakiwa wamewatanguliza washtakiwa mbele.

Alidai kuwa watu hao walikuwa wamempeleka Mketo (wakati wa uhai wake), lakini hakuwa anajitambua kutokana na majeraha mbalimbali mwilini huku akitokwa damu puani na masikioni.

"Nilituliza jazba ya wananchi, nikawaweka watuhumiwa mahabusu kwa usalama wao. Nikaandika fomu namba tatu kwa ajili ya kumpeleka majeruhi kutibiwa... niliwaweka washtakiwa mahabusu kwa sababu wananchi walikuwa wanapiga kelele kwamba watafungua bucha dhidi yao," alidai shahidi huyo na kuongeza:

"Nilimhoji mshtakiwa Rwambo kuhusu tukio hilo, alinieleza kwamba yeye na Mketo ni marafiki na kwamba siku hiyo walikuwa wote
kwenda kwa mshtakiwa wa pili, ambaye ni mfanyabiashara wa pombe za kienyeji ikiwamo gongo."

Kachero huyo alidai kuwa wakiwa hapo nyumbani kwa mshtakiwa wa pili, Rwambo alitoka kwenda chooni aliporejea hakuiona simu yake ya mkononi aina ya Nokia na ndipo ugomvi ulipoanzia.

Alidai kuwa baada ya tukio la kupotea simu, mshtakiwa wa kwanza alitaka kumpeleka polisi, lakini mshtakiwa wa pili alimzuia kwa sababu anafanya biashara haramu ya gongo angesumbuliwa na askari.

Alidai kuwa Aprili 23, 2012 alidamka kwenda kumwangalia majeruhi Mketo kituo cha afya Kibiti alimkuta akiwa na hali mbaya sana.

Alidai kuwa Aprili 28, 2012 Mketo alifariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikohamishiwa baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya.

Awali washtakiwa walifunguliwa mashtaka ya kujeruhi mwili, lakini baadaye hati ya mashtaka ilibadilika na kuwa ya mauaji.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Elizabeth Olomi, ulifunga ushahidi wake.

Mahakama imewaona wana kesi ya kujibu watapanda kujitetea kizimbani leo.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Aprili 22, 2012 eneo la Kibiti,Wilaya ya Rufiji walimuua kwa makusudi Mketo.

0 comments:

Post a Comment