Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) inapenda
kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL)
iliyotolewa kwenye magazeti ya Mwananchi na Uhuru ya tarehe 15/11/2017.
Gazeti la Mwananchi liliandika, “Serikali ‘yaiua’ rasmi TTCL na gazeti
la Uhuru liliandika,“TTCL ‘bye’ ‘bye’. Vichwa hivi vya habari
vimewachanganya wasomaji na kuleta taharuki kwa wateja na wafanyakazi wa
TTCL, wadau wa Sekta ya Mawasiliano na wananchi kwa ujumla.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewasilisha
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania katika mkutano wa
Tisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba, 2017
mjini Dodoma. Bunge lilijadili na kupitisha Muswada na kutungwa kuwa
Sheria itakayoanzisha Shirika la Mawasiliano Tanzania. Madhumuni ya
Muswada yalikuwa ni kuanzisha Shirika la Umma la Mawasiliano nchini kwa
ajili ya kulinda usalama wa nchi, kukuza uchumi na kutoa huduma za
mawasiliano kwa ubora unaotakiwa. Pia, kulipa Shirika la Mawasiliano
jukumu la kusimamia miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano nchini.
Sheria
mpya itaiwezesha TTCL kutekeleza majukumu yake kama Shirika la
Mawasiliano nchini. Hizi ni jitihada za Serikali kuimarisha TTCL na sio
kuiua. TTCL bado ipo na itaendelea kutekeleza majukumu yake kama Shirika
la Mawailiano nchini. Shirika litaendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa
ubora na ufanisi zaidi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
17 Novemba, 2017
0 comments:
Post a Comment