Wednesday 6 December 2017

Mjumbe wa UN aelekea Korea Kaskazini kumaliza mzozo na Marekani

Mjumbe wa umoja wa mataifa umeelekea Pyongyang mchana wa leo kwa ziara isiyo ya kawaida, kwa lengo la kujaribu kuuzima mvutano kati ya taifa hilo na Marekani kufuatia mpango wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini

Mvutano mkali unaoendelea kati ya Marekani na Korea kaskazini kutokana na mpango wake wa silaha za nyuklia unaendeleza hali ya wasiwasi katika eneo la Korea na duniani kwa ujumla. Kutokana na hali hiyo, umoja wa mataifa umetuma ujumbe wake kwenda Korea kaskazini kujaribu kutuliza hali.
Jeffrey Feltman - mshauri wa umoja wa mataifa katika maswala ya kisiasa Jeffrey Feltman - mshauri wa umoja wa mataifa katika maswala ya kisiasa
Ziara ya Jeffrey Feltman – mshauri wa umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa, ni ya kwanza kufanywa na mwanadiplomasia wa cheo cha juu wa umoja huo tangu mwaka 2010. Haya yanajiri siku chache baada ya Korea Kaskazini kusema imefanikiwa katika jaribio la kombora jipya linaloweza kufikia Marekani.
Ziara hii pia inakuja siku moja baada ya Marekani na Korea kusini kuanza mazoezi ya pamoja na  kijeshi, kuonyesha utayarifu wa kukabiliana na kitisho cha Korea kaskazini.
Mnamo siku ya Jumatatu, Feltman, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kisiasa, aliwasili nchini China ambako alikutana na makamu waziri wa maswala ya kigeni wa China mjini Beijing.
China, ambayo ni mshirika wa pekee wa kidiplomasia na kijeshi wa Korea Kaskazini, imetoa wito kwa Marekani kusitisha mazoezi hayo kijeshi,na kuitaka pia Korea ya Kaskazini isitishe majaribio ya makombora ili kutuliza hali  hiyo tete.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema, akiwa Korea Kaskazini Feltman  atajadili juu ya  "maswala ya maslahi ya pamoja na yenye umuhimu zaidi" na viongozi wa taifa hilo la kikomunisti pamoja na kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jung-Un.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeliwekea taifa hilo lililotengwa la Korea kaskazini, vikwazo zaidi  kufuatia kuendeleza majaribio yake ya makombora na silaha za nyuklia ambayo yameitia wasiwasi Marekani na washirika wake Korea Kusini na Japan.

0 comments:

Post a Comment