Wednesday 27 December 2017

Wakandarasi walioshindwa kukamilisha miradi kukiona


Naibu waziri wa Nishati nchini Bi Subira Mgalu amesema wakandarasi ambao wameshindwa kukamilisha miradi ya usambazaji wa umeme vijijini Awamu ya Pili (REA II), watachukuliwa hatua za kisheria na serikali.
Wakandarasi hao ni kampuni ya Derm inayosambaza miundombinu ya umeme katika wilaya za Handeni, Kilindi, Korogwe na Lushoto, Kampuni za Radi, Njarita na Aguila zinazosambaza umeme wilaya za Mkinga, Pangani, Muheza na Bumbuli na kampuni ya Namis Co-operate Ltd inayosambaza miundombinu ya umeme katika wilaya zote za Tanga.
Naibu Waziri alisema kuwa wakandarasi waliopewa kazi ya kusambaza miundombinu ya kusambaza umeme vijijini kupitia REA Awamu ya Pili, walilipwa malipo yote, hivyo walipaswa kukamilisha miradi yote kwa wakati.
Aidha, aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA Awamu ya Tatu, kuongeza kasi katika miradi ya usambazaji wa umeme vijijini na kuongeza kuwa kipaumbele kitolewe katika taasisi kama shule, vituo vya afya, zahanati, visima vya maji ili wananchi waanze kufurahia huduma za jamii. Aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA katika mikoa miwili tofauti, kuhakikisha kuwa kasi inakwenda kwa kiwango sawa na kuepuka kuwekeza nguvu kwenye mkoa mmoja tu.

0 comments:

Post a Comment