Thursday 1 February 2018

Kamata kamata yaanza kuwanasa wapinzani Kenya


Kamata kamata huko Kenya imeanza kushuhudiwa baada ya kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga kujiapisha kama rais wa wananchi hapo Jumanne.
Wakili Tom Kajwang aliyesimamia hatua hiyo ya kujiapisha Raila Odinga ametiwa nguvuni huku Serikali ikisema kuwa watu wengi watakamatwa. Wakati huo huo serikali imesema wakenya wataendelea kukosa kutizama vituo vitatu vya televisheni hadi uchunguzi utakapokamilika.
Siku moja baada ya Raila Odinga kujiapisha kuwa rais wa wananchi wa Kenya serikali imemkamata wakili Tom Kajwang aliyesimamia kiapo cha Odinga. Hata hivyo hapajatolewa taarifa zozote kuhusu sababu za kumtia nguvuni.
Wakili huyo ambaye ni mwanachama wa Muungano wa NASA alikamatwa na maafisa wa ujasusi alipokuwa mahakamani. Waziri wa usalama Fred Matiang'i aliyetaja hafla hiyo kuwa kinyume cha sheria amesema uchunguzi unaendelea na kuwa watu kadhaa watatiwa nguvuni.
Vituo vya televisheni vitazimwa hadi uchunguzi ukamilike
Waziri Matiangi amedokeza kuwa sasa wanavichunguza vituo vya televisheni vya KTN, Nation Media Group pamoja na Citizen ambavyo amevitaja kuwa huenda vilikuwa na nia ya kushirikiana na wahalifu.
Fred Matiangi vorne links (Imago/Xinhua Afrika) Waziri wa usalama wa ndani Kenya, Fred Matiang'i (kushoto) amesema wengi watakamatwa
"Almuradi uchunguzi huo unaendelea kuna baadhi ya hatua ambazo zitasalia," alisema Matiang'i, "kwa mfano vituo hivyo vya televisheheni vitaendelea kuzimwa hadi uchunguzi huo ukamilike,” aliongeza waziri huyo.
Kadhalika serikali ya Kenya inasema kuondolewa kwa jeshi la polisi hapo jana katika uwanja wa Uhuru park ulikuwa mkakati wa makusudi  kuepusha umwagikaji wa damu baada ya kupata taarifa za kijasusi kuwa kulikuwa na wahalifu waliojikita chini ya mwavuli wa Muungano wa NASA.
"Hizo zilikuwa juhudi zilizopangwa vizuri zilizolenga kuzusha makabiliano na jeshi la polisi ili kusababisha umwagikaji wa damu ya wananchi wasio na hatia,” alisema Waziri huyo wa usalama wa ndani.

0 comments:

Post a Comment